
DODOMA: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameitaka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Kazi kusimamia sheria na kutenda haki kwa waajiri na waajiriwa bila upendeleo, chuki wala hila katika maamuzi yake.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo, Novemba 2, 2026, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi wateule iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, ambapo amempongeza Jaji mstaafu Wilfred Sobera, Mwenyekiti wa tume hiyo, pamoja na makamishna walioapishwa.
Amesema tume hiyo inapaswa kuhakikisha maamuzi yake yanazingatia sheria na ushahidi uliopo, akibainisha kuwa baadhi ya maamuzi yanapowasilishwa kwake kupitia rufaa huwa na hoja zinazohitaji kukubaliwa au kukataliwa.

Amesisitiza kuwa hali hiyo inaonesha umuhimu wa viongozi wa tume kuwa makini, waadilifu na wenye weledi katika kushughulikia migogoro inayojitokeza baina ya waajiri na waajiriwa.
Aidha, Rais Samia amesema ongezeko la uwekezaji na kuingia kwa kampuni binafsi nchini kumeongeza shughuli za kiuchumi pamoja na uwezekano wa kujitokeza kwa migogoro ya kikazi, hivyo tume inapaswa kuhakikisha pande zote zinapata haki kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kufuatilia na kujibu shutuma zinazotolewa dhidi ya Tanzania kuhusu masuala ya haki za binadamu, kwa kuzingatia ukweli na hali halisi ya mambo.
Akizungumza katika hafla hiyo hiyo, Rais Samia amesema tafsiri ya masuala ya haki za binadamu katika dunia ya sasa imekuwa na changamoto, akibainisha kuwa baadhi ya nchi hukosolewa kutokana na mitazamo ya wengine, huku nyingine zikikabiliwa na tuhuma bila kupewa uzito unaolingana.
Amewataka makamishna wa tume hiyo kutumia uwezo na mamlaka yao kufuatilia taarifa zinazochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali kuhusu Tanzania, kuzichambua na kutoa majibu yanayozingatia ukweli.
Amesisitiza kuwa jukumu la tume hiyo halipaswi kuishia kusubiri malalamiko kutoka kwa wananchi wanaodai kuvunjiwa haki zao, bali linapaswa pia kujumuisha ufuatiliaji wa masuala ya utawala bora na namna haki za binadamu zinavyotekelezwa nchini.
Rais Samia amesema matarajio yake ni kuona tume hiyo ikitekeleza majukumu yake kwa upana, ikiwemo kushughulikia malalamiko ya wananchi, kufuatilia masuala ya utawala bora na kutoa ufafanuzi kuhusu hoja zinazotolewa kimataifa kuhusiana na hali ya haki za binadamu nchini.
Maelekezo hayo yametolewa wakati wa kuwaapisha viongozi wateule wa taasisi hizo, yakilenga kusisitiza wajibu wa tume hizo katika kusimamia haki, uwajibikaji na utawala bora nchini.