
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewaonya watu wanaodaiwa kuhamasishana ndani na nje ya Mkoa huo kwa lengo la kufanya fujo, vurugu na hujuma mbalimbali Novemba 6, 2026.
Jeshi hilo limesema halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kujihusisha na mipango hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 03,2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, SACP Jumanne J. Muliro, amesema Jeshi hilo linaendelea kufuatilia kwa karibu kundi hilo na kwamba haitavumilia viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani katika Jiji la Dar es Salaam.
Amesema jeshi hilo litachukua hatua za haraka na za kisheria dhidi ya mipango yoyote itakayolenga kuvuruga amani, huku akiwataka wananchi kuheshimu utaratibu uliowekwa na Mahakama katika kufuatilia mashauri mbalimbali.
Katika hatua nyingine, SACP Muliro amesema katika kipindi cha Oktoba mwaka huu, Polisi Dar es Salaam ilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 67 wanaotuhumiwa kujihusisha na makosa mbalimbali ya jinai na kupata baadhi ya vitu vilivyoibwa.
Kuhusu mafanikio ya mashauri ya jinai yaliyofikishwa mahakamani kupitia Ofisi ya Mashitaka, Kamanda Murilo amesema baadhi ya watuhumiwa wamepatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali vya jela.
Muliro amewashukuru wananchi wanaojitokeza kwa wingi kushiriki kampeni ya ‘Ongea na Kamanda’ inayoendelea jijini Dar es Salaam, akisema inalenga kujenga ushirikiano kati ya Polisi na wananchi katika kujadili changamoto za kiusalama katika maeneo yao na kuzitafutia ufumbuzi.