×

Rita Moreno Afichua Siri ya Kutunza Tuzo Zake Zote Katika Chumba Maalumu Nyumbani

Mwigizaji mkongwe wa Hollywood, Rita Moreno, mwenye umri wa miaka 94, amefichua kuwa ana chumba maalumu nyumbani kwake ambacho hutumia kutunza tuzo zote alizojinyakulia katika safari yake ya zaidi ya miaka 80 kwenye tasnia ya burudani.

Moreno ametoa kauli hiyo alipohudhuria hafla ya 2026 Día de Muertos Gala iliyofanyika jijini Los Angeles, Marekani, Oktoba 27, ambapo alizungumza kuhusu namna anavyohifadhi kumbukumbu za mafanikio yake.

“Nimeshinda vitu vingi sana. Tuzo zangu ziko nyumbani, nina chumba kimoja ambacho zote zimewekwa,” alisema Moreno.

Mwigizaji huyo ni miongoni mwa wasanii wachache duniani waliotunukiwa heshima ya EGOT, inayotolewa kwa watu waliofanikiwa kushinda tuzo kuu nne za burudani nchini Marekani, ambazo ni Emmy, Grammy, Oscar na Tony.

Alikamilisha mafanikio hayo mwaka 1977 baada ya kushinda tuzo ya Primetime Emmy kutokana na ushiriki wake katika kipindi cha televisheni cha The Muppet Show.

Safari yake ya mafanikio ilianza mwaka 1962 aliposhinda tuzo ya Oscar ya mwigizaji bora msaidizi kupitia filamu ya West Side Story Mwaka 1972 alitwaa tuzo ya Grammy kupitia kazi yake ya The Electric Company, kabla ya kushinda tuzo ya Tony mwaka 1975 kutokana na uigizaji wake katika tamthilia ya The Ritz.

Mwaka 1978 aliongeza tuzo nyingine ya Emmy baada ya kutambuliwa kama mwigizaji bora wa kike katika kipindi cha televisheni kupitia nafasi yake katika tamthilia ya The Rockford Files.

Mbali na tuzo hizo nne kubwa, Moreno amepokea heshima na tuzo nyingine nyingi katika kipindi chote cha kazi yake iliyohusisha maigizo ya jukwaani na filamu.

Kwa sasa, mwigizaji huyo anajiandaa kutimiza miaka 95 ifikapo Desemba 11, 2026, ambapo amesema anatarajia kusherehekea siku hiyo kwa kupata chakula cha jioni pamoja na marafiki zake wa karibu.

Akizungumzia hatua hiyo ya maisha yake, Moreno amesema anashangazwa na safari yake ya kufikia umri huo na kujiona bado anaendelea kuwa imara.

Pia amesema anajisikia mwenye heshima kubwa kuwa miongoni mwa wasanii wachache waliosalia kutoka kizazi cha dhahabu cha Hollywood (Hollywood’s Golden Age).

Amesema anafurahia kuendelea kuwa hai na kupata nafasi ya kushuhudia safari ndefu ya maisha yake katika tasnia ya burudani.

Leave a Comment