×

Uchaguzi wa Marekani leo; Trump Kupata Pigo, Democratic Yalenga Kudhibiti Congress

Wamarekani leo, Jumanne Novemba 3, 2026, wanapiga kura katika uchaguzi wa katikati ya muhula unaotarajiwa kuwa na athari kubwa katika mustakabali wa kisiasa wa Marekani, huku chama cha Republican cha Rais Donald Trump kikikabiliwa na uwezekano wa kupoteza udhibiti wa Bunge la Congress.

Katika uchaguzi huo, wapiga kura wanatarajiwa kuamua hatima ya viti vyote 435 vya Baraza la Wawakilishi pamoja na viti 35 kati ya 100 vya Seneti, katika kinyang’anyiro kinachoweza kubadili uwiano wa madaraka nchini humo kwa kipindi kilichosalia cha utawala wa Trump.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na shirika la habari la Reuters kwa kushirikiana na Ipsos unaonesha kuwa wagombea wa chama cha Democratic wanaongoza kwa tofauti ya asilimia nane dhidi ya wagombea wa Republican, hali inayoongeza presha kwa chama tawala.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanakiona chama cha Democratic kuwa na nafasi kubwa ya kurejesha udhibiti wa Baraza la Wawakilishi, ingawa ushindani wa kuwania udhibiti wa Seneti unatarajiwa kuwa mkali zaidi.

Iwapo Republican kitapoteza udhibiti wa mojawapo ya vyumba vya Congress, hatua hiyo inaweza kudhoofisha uwezo wa Rais Trump kupitisha miswada ya sheria na kutekeleza ajenda yake ya kisiasa.

Aidha, ushindi wa Democratic unaweza kukipa chama hicho nafasi kubwa ya kuisimamia na kuichunguza serikali ya Trump kupitia kamati za Bunge, pamoja na kuibua mijadala kuhusu sera na maamuzi ya utawala wake.

Kwa upande wa Seneti, matokeo ya uchaguzi yana umuhimu wa kipekee kutokana na mamlaka ya chumba hicho katika kuthibitisha uteuzi wa majaji wa mahakama za shirikisho, wakiwemo majaji wa Mahakama ya Juu ya Marekani.

Hivyo, uchaguzi huo hautakuwa tu kipimo cha umaarufu wa Rais Trump na chama chake, bali pia utakuwa mtihani muhimu wa uwiano wa madaraka na mwelekeo wa siasa za Marekani kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2028.

Leave a Comment