
Wizara ya Sheria ya Marekani (Department of Justice – DOJ) imetangaza kufunguliwa kwa mashtaka dhidi ya watu 63 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo mbalimbali vya ukiukwaji wa sheria za uchaguzi nchini humo, ikiwemo kupiga kura kinyume cha sheria na kufanya udanganyifu katika usajili wa wapiga kura.
Taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo Novemba 2, 2026, imeeleza kuwa miongoni mwa watuhumiwa hao wapo raia wanne wa kigeni ambao kwa mujibu wa mamlaka hiyo wanaishi nchini Marekani bila kuwa na vibali halali vya ukaazi.
Kwa mujibu wa DOJ, makosa yanayohusishwa na watuhumiwa hao ni pamoja na raia wasio na uraia wa Marekani kushiriki katika uchaguzi wa Shirikisho, kutoa taarifa za uongo kuhusu uraia wa Marekani ili kujisajili kama wapiga kura na kuwasilisha maombi ya usajili wa wapiga kura kwa njia za udanganyifu.

Akizungumzia hatua hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Todd Blanche, amesema tangazo hilo linaashiria ongezeko kubwa la hatua za kukabiliana na udanganyifu wa uchaguzi tangu Rais Donald Trump arejee madarakani.
Blanche amesisitiza kuwa Wizara ya Sheria itaendelea kuchunguza na kuwafikisha mahakamani wote watakaobainika kukiuka sheria za uchaguzi ili kurejesha imani ya wananchi katika mfumo wa uchaguzi nchini humo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika kipindi cha wiki tisa zilizopita, Wizara hiyo imewafungulia mashtaka raia 195 wa kigeni katika majimbo 25 kwa makosa yanayohusiana na upigaji kura na usajili wa wapiga kura kinyume cha sheria.
Hata hivyo, Wizara ya Sheria imeweka wazi kuwa mashtaka yaliyotangazwa ni tuhuma ambazo bado zinapaswa kuthibitishwa mahakamani, hivyo watuhumiwa wote wanachukuliwa kuwa hawana hatia hadi pale watakapothibitika kuwa na hatia kwa mujibu wa sheria.