
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Elie Mpanzu, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027, huku kocha wa timu hiyo, Steven Barker, akitwaa tuzo ya Kocha Bora wa mwezi huo.
Mpanzu amefanikiwa kutwaa tuzo hiyo baada ya kuonyesha kiwango bora cha mchezo, aki washinda Iddi Selemani wa Azam FC na Nathaniel Chilambo wa Simba SC, ambao pia waliingia fainali ya tuzo hiyo.
Katika michezo mitatu iliyochezwa mwezi Oktoba, Mpanzu alifunga mabao matatu na kuisaidia Simba SC kupata matokeo mazuri kwenye ligi.

Kwa upande wa tuzo ya Kocha Bora, Steven Barker aliwashinda Florent Ibenge wa Azam FC na Juma Mgunda wa Namungo FC, baada ya kuiongoza Simba SC kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo na kupanda kutoka nafasi ya pili hadi ya kwanza katika msimamo wa ligi.
Kamati ya Tuzo pia imetangaza mabao matatu bora ya mwezi Oktoba, ambayo yatapigiwa kura na mashabiki ili kumpata mshindi. Mabao hayo yamefungwa na Hassan Mubiru wa Azam FC dhidi ya Mbeya City, Elie Mpanzu wa Simba SC dhidi ya Young Africans na Selemani Bwenzi wa Simba SC dhidi ya Mashujaa FC.

Aidha, Jackson Mwendwa wa Tanzania Prisons ametangazwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja wa mwezi Oktoba, kutokana na usimamizi mzuri wa maandalizi ya uwanja na masuala yanayohusu miundombinu ya michezo.
Katika Ligi ya Championship ya NBC, Ramadhan Kalanje wa KMC amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba baada ya kuwashinda Abdulkariim Segeja wa Kigamboni na Hamdan Ally wa Transit Camp.
Kwa upande wa tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Oktoba katika Championship, Awadh Juma wa Mtibwa Sugar ndiye aliyeibuka mshindi, akiwashinda Habibu Kondo wa Bandari na Mohamed Muya wa KMC.
Taarifa hiyo imetolewa Novemba 5, 2026 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
