
DAR ES SALAAM: Ulinzi umeimarishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, wakati hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ikitarajiwa kutolewa leo, Novemba 6, 2026.
Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa kuanzia saa tatu asubuhi (9:00), huku Jeshi la Polisi likiongeza ulinzi katika maeneo ya nje ya mahakama hiyo kuhakikisha usalama wakati wa shughuli za utoaji wa hukumu.
Ni siku 577 tangu Lissu alipokamatwa Aprili 9, 2025, na baadaye kufunguliwa mashtaka ya uhaini, katika kesi ambayo imechukua takribani mwaka mmoja na miezi saba kufikia hatua ya kusubiri uamuzi wa mahakama.
Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, ambapo upande wa mashtaka unadai kuwa alitoa matamshi Aprili 3, 2025, katika makao makuu ya CHADEMA jijini Dar es Salaam, yaliyokuwa na lengo la kuhamasisha wananchi kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa matamshi hayo yalilenga kuishinikiza Serikali na kwamba ushahidi uliowasilishwa mahakamani, ukiwemo wa mashahidi 17 wa upande wa mashtaka, ulithibitisha tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo, Lissu amekuwa akipinga tuhuma hizo, akieleza katika utetezi wake kuwa matamshi aliyotoa hayakufikia kiwango cha kosa la uhaini na kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi yake kwa mujibu wa sheria.
Mnamo Agosti 21, 2026, Mahakama ilitoa uamuzi kuwa Lissu ana kesi ya kujibu na kumtaka kuwasilisha utetezi wake. Baadaye aliwasilisha utetezi pamoja na mashahidi watano kabla ya pande zote mbili kuhitimisha hoja zao.
Mnamo Septemba 29, 2026, jopo la majaji watatu lilihitimisha kusikiliza hoja za mwisho za pande zote na kupanga kutoa hukumu Novemba 6, 2026.
Jopo hilo linaongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Katika hatua hiyo ya mwisho, upande wa mashtaka uliomba mahakama imtie Lissu hatiani, ukisisitiza kuwa ushahidi uliowasilishwa umethibitisha shtaka hilo. Kwa upande mwingine, Lissu aliiomba mahakama itupilie mbali shtaka hilo kwa maelezo kuwa halijathibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.
Leo, macho ya wananchi, viongozi wa kisiasa, wafuasi wa CHADEMA na wadau mbalimbali yanaelekezwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kusubiri uamuzi wa majaji kuhusu hatma ya kesi hiyo.
Hukumu hiyo inasubiriwa kwa karibu kutokana na uzito wa shtaka linalomkabili Lissu pamoja na athari zake za kisheria. Kosa la uhaini linaweza kubeba adhabu kali, ikiwemo adhabu ya kifo, endapo mahakama itatoa hukumu ya kumtia hatiani na kuamua adhabu hiyo kwa mujibu wa sheria.
Uamuzi wa mahakama unatarajiwa kuweka hitimisho la hatua hii ya kesi iliyofuatiliwa kwa karibu nchini na nje ya Tanzania.