
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limewakamata watu 16 wanaotuhumiwa kujihusisha na makosa mbalimbali ya uhalifu, yakiwemo wizi wa pikipiki, televisheni, vifaa vya umeme majumbani na kuuza mali za wizi katika Wilaya ya Karagwe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Novemba 10, 2026, watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni maalumu iliyofanyika kuanzia Septemba 2026 hadi Novemba 10, mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti uhalifu na kuimarisha usalama wa wananchi.
Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni Baraka Mgalula (23), Joseph Domonik (38), Azili Abasi (29), Athuman Chiza (30), Emanuel Evalist (35), Mudashiru Issa Mhaya (45), Nestory Joseph (34), Juvent Jonas (26), Godlove Mtoka (31), Msafiri Obadi (27), Dominick Anthony (45), Yuhai Ngoma (32), Daniel Costantine (32), Anisia Ernest (28), Twaibu Adamu (24) na Amodius Paul Nyambo (26).
Katika operesheni hiyo, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata mali mbalimbali zinazodaiwa kuhusishwa na uhalifu huo, zikiwemo pikipiki 10 za aina tofauti, televisheni 18, sabhufa saba, spika 14, kompyuta mpakato moja, godoro moja pamoja na mtungi wa gesi na simu mbalimbali.
Jeshi la Polisi limesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya jeshi hilo na wananchi wa Mkoa wa Kagera, ambao wamekuwa wakitoa taarifa za uhalifu na uhalifu unaopangwa pamoja na ushahidi mahakamani pale unapohitajika.
Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
