×

Lissu Aanza Mchakato wa Rufaa Kupinga Hukumu ya Miaka Minne Jela

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, ameanza rasmi mchakato wa kupinga hukumu ya kifungo cha miaka minne jela aliyopewa na Mahakama Kuu ya Tanzania Novemba 6, 2026, baada ya kupatikana na hatia ya kosa la uchochezi.

Taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa timu ya mawakili wake tayari imewasilisha hati ya kusudio la kukata rufaa Novemba 7, 2026, ikiwa ni hatua ya awali kuelekea kuipeleka kesi hiyo katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

Wakili wa Lissu, Dkt. Rugemeleza Nshala, pamoja na timu nyingine ya mawakili, wanaendelea na maandalizi ya kisheria huku wakisubiri kupatiwa nakala ya hukumu na mwenendo mzima wa kesi ili kukamilisha hoja zitakazowasilishwa katika rufaa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mmoja wa mawakili wake, William Maduhu, maandalizi ya rufaa hiyo yamefikia takribani asilimia 50, huku timu ya utetezi ikieleza kuwa imebaini hoja zaidi ya 10 zinazoweza kupingwa katika uamuzi wa mahakama.

Miongoni mwa hoja zinazotarajiwa kuangaliwa ni mamlaka ya Mahakama Kuu kusikiliza na kutoa hukumu ya kosa la uchochezi, pamoja na suala la haki ya mshtakiwa kupewa nafasi ya kutosha kujiandaa kujitetea dhidi ya kosa ambalo hakuwasilishiwa kama shtaka la awali.

Lissu awali alikuwa akikabiliwa na shtaka la uhaini lililotokana na kauli alizodaiwa kutoa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, kuhusu haja ya kufanyika kwa mageuzi ya uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Hata hivyo, katika hukumu iliyotolewa Novemba 6, 2026, majaji watatu wa Mahakama Kuu walimkuta hana hatia ya uhaini baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka hilo, lakini wakamtia hatiani kwa kosa la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela.

Uamuzi huo ulifuatia kesi iliyodumu kwa takribani miezi 19, huku Lissu akiwa amekaa mahabusu kwa siku 577 tangu alipokamatwa Aprili 2025.

Kwa upande mwingine, mawakili wake wameeleza kuwa baada ya kukamilisha rufaa, wanatarajia pia kuwasilisha maombi ya dhamana wakati rufaa hiyo ikiendelea kusubiriwa.

Hatua hiyo inaashiria kuanza kwa hatua nyingine ya kisheria katika kesi inayofuatiliwa kwa karibu na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania.

Leave a Comment