
MOSCOW, URUSI: Balozi wa Urusi nchini Marekani, Alexander Darchiev, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 66, katika kipindi ambacho Moscow na Washington zinaendelea na juhudi za kidiplomasia kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo vita vya Ukraine.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imethibitisha kifo cha mwanadiplomasia huyo kilichotokea Jumatano, Novemba 11, 2026, mjini Moscow.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na wizara hiyo, Darchiev alifariki dunia ghafla, huku msemaji wa wizara hiyo, Maria Zakharova, akieleza baadaye kuwa kifo chake kilitokana na ugonjwa wa muda mrefu, bila kufafanua aina ya ugonjwa huo.
Darchiev aliteuliwa kuwa balozi wa Urusi nchini Marekani mwezi Machi 2025 na Rais Vladimir Putin, akiwa na jukumu la kuimarisha mahusiano kati ya mataifa hayo mawili yaliyokuwa na mvutano wa kidiplomasia.
Kabla ya uteuzi huo, aliwahi kuwa balozi wa Urusi nchini Canada kuanzia mwaka 2014 hadi 2021, pamoja na kushika nyadhifa mbalimbali katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, hususan zinazohusu masuala ya Amerika Kaskazini.
Pia, Februari 2025, Darchiev aliongoza ujumbe wa Urusi katika mazungumzo na Marekani yaliyofanyika Istanbul, Uturuki, yaliyolenga kujadili masuala ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Kifo chake kimetokea wakati ambapo uhusiano wa Urusi na Marekani unaendelea kuwa na changamoto kutokana na vita vya Ukraine, licha ya juhudi za pande hizo kutafuta njia za mazungumzo na kuboresha mawasiliano ya kidiplomasia.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imemuelezea Darchiev kama mwanadiplomasia mahiri, kiongozi mwenye uzoefu na mshauri aliyekuwa na mchango mkubwa katika masuala ya sera za nje za nchi hiyo.
Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu tarehe ya mazishi yake.