
Msanii wa muziki kutoka Hispania, Rosalía, ameibuka miongoni mwa vinara wa tuzo za 27 za Latin Grammy Awards baada ya kutwaa tuzo ya Albamu Bora ya Mwaka (Album of the Year) kupitia albamu yake ya ‘Lux’, katika hafla iliyofanyika jijini Las Vegas, Marekani.
Ushindi huo umeongeza rekodi ya Rosalía katika kipengele hicho na kumfanya kufikisha mara tatu za kutwaa tuzo ya Albamu Bora ya Mwaka, baada ya awali kufanya hivyo kupitia albamu zake za ‘El Mal Querer’ mwaka 2018 na ‘Motomami’ mwaka 2022.
Mbali na ushindi huo, Rosalía pia alihusika katika mafanikio ya wimbo ‘La Perla’, uliotwaa tuzo ya Wimbo Bora wa Mwaka (Song of the Year) pamoja na Wimbo Bora wa Pop (Best Pop Song), akiwa ameshirikiana na Yahritza y Su Esencia.
Tuzo hizo zimewakutanisha wasanii mbalimbali kutoka katika mataifa ya muziki wa Kilatini, huku kila mmoja akishindania kutambuliwa kupitia kazi zake katika vipengele tofauti.
Katika kipengele cha Msanii Bora Chipukizi (Best New Artist), Aria Vega ndiye aliyeibuka mshindi, huku Alejandro Sanz akitwaa tuzo ya Albamu Bora ya Kisasa ya Pop kupitia kazi yake ya ‘¿Y Ahora Qué +?’.

Kwa upande wa muziki wa Reggaeton na Urbano, Karol G alifanikiwa kutwaa tuzo ya Utendaji Bora wa Reggaeton kupitia wimbo ‘Verano Rosa’, akimshirikisha Feid, pamoja na Albamu Bora ya Muziki wa Urbano kupitia albamu yake ya ‘Tropicoqueta’.
Wasanii wengine waliofanikiwa ni pamoja na J Noa na Trooko, waliotwaa tuzo ya Wimbo Bora wa Rap/Hip Hop kupitia ‘Antisistema’, huku Bizarrap na Daddy Yankee wakishinda kipengele cha Wimbo Bora wa Urbano kupitia ‘Daddy Yankee: Bzrp Music Sessions Vol. 0/66’.
Katika muziki wa Rock, Fito Páez alitwaa tuzo ya Albamu Bora kupitia ‘Shine’, huku kundi la The Warning likishinda Wimbo Bora wa Rock kupitia kazi yao ya ‘Ego’.
Kwa upande wa muziki wa Salsa, Luis Enrique alitwaa tuzo ya Albamu Bora kupitia ‘El Alma En Clave’. Naye Carlos Vives akafanikiwa katika kipengele cha Albamu Bora ya Cumbia/Vallenato kupitia ‘El Último Disco Vol. 1’.
Washindi wengine ni Luis Enrique, De La Ghetto na wasanii wenzao kupitia wimbo ‘Nombre y Apellido’, uliotwaa tuzo ya Wimbo Bora wa Muziki wa Tropical.
Katika vipengele vingine, Camila Fernández alishinda Albamu Bora ya Ranchera/Mariachi kupitia ‘La Fernández’, Silvana Estrada akatwaa Wimbo Bora wa Mwimbaji na Mtunzi kupitia ‘Dime’, huku Gonzalo Rubalcaba akipata tuzo ya Albamu Bora ya Latin Jazz/Jazz kupitia ‘Gonzalo Plays Pino’.
Mafanikio ya Rosalía kupitia ‘Lux’ yanaongeza ukurasa mwingine katika safari yake ya muziki wa kimataifa, huku ushindi wake ukiendelea kuimarisha nafasi yake katika tasnia ya muziki wa Kilatini.
Hata hivyo, usiku huo umeonesha pia ushindani na vipaji mbalimbali vya wasanii wa muziki wa Kilatini katika mitindo tofauti, kuanzia Pop, Reggaeton, Rap, Rock hadi Salsa.