×

Waziri Mkuu Mwigulu: Rais Samia Anastahili Kutambuliwa Kama Malkia wa Nguvu

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi zinapaswa kupewa kipaumbele ili kujenga familia imara na jamii yenye maendeleo.

Dkt. Mwigulu amesema wanawake wanapopata fursa za kiuchumi, elimu na mitaji, manufaa yake hayaishii kwao pekee bali huenea katika familia na jamii nzima ya Watanzania.

Waziri Mkuu ameyasema hayo usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 15, 2026 alipokuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya Tuzo za Malkia wa Nguvu Tanzania 2026 zilizoandaliwa na Clouds Media Group, katika ukumbi wa Ocean View Arena, Kawe jijini Dar es Salaam, ambapo amesema uwezeshaji wanawake unahitaji juhudi za pamoja kutoka serikalini, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Dkt. Mwigulu ameongeza kuwa Serikali, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan, kama sehemu ya kumuinua mwanamke, imechukua hatua kubwa katika kuimarisha elimu na ustawi wa mtoto wa kike, ikiwemo ujenzi wa shule maalumu za wasichana katika mikoa mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu amesema kutokana na hatua hizo, Rais Dkt. Samia anapaswa kutambuliwa kama Malkia wa Nguvu kwani mchango wake katika kuwawezesha wasichana na wanawake ni mkubwa. “Katika miaka yake minne mpaka mitano iliyopita, Mheshimiwa Rais amejenga shule maalum za wasichana kwa kila mkoa, kwa mpigo. Tangu uhuru haikuwahi kutokea hiyo. Tumekuwa na shule na hata hizo maalum tumekuwa nazo, lakini haikuwahi kutokea kujenga shule maalum kila mkoa kwa ajili ya wasichana, yenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watoto wa kike elfu moja. Hii ni hatua kubwa sana,” amesema Waziri Mkuu.

Leave a Comment