Benki ya NMB imewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa malengo na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji ili kuimarisha ustawi wao wa kifedha na kujenga mitaji ya muda mrefu. Wito huo umetolewa katika warsha ya From Saving to Smart Investing (Akiba Hadi Uwekezaji) iliyoandaliwa na Bridge Consult kwa udhamini wa NMB katika Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Wawekezaji wa NMB, Mark Hiza, aliwahimiza wananchi kutathmini hali zao za kifedha na kuweka malengo ya miaka mitatu, mitano na kumi. Alieleza kuwa kupitia NMB Mkononi, wateja wanaweza kusimamia akaunti na kufanya miamala kwa urahisi, huku vikundi vya kuweka na kukopa (vikoba) vikiwezeshwa kufungua na kusimamia akaunti kidijitali ili kuongeza usalama na uwazi katika usimamizi wa fedha. 

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Huduma za Kibenki kwa Wateja Binafsi wa NMB, Zuberi Bani, alisisitiza umuhimu wa elimu ya fedha, hususan kwa vijana, katika kupanga matumizi, kuweka akiba na kutumia huduma za kidijitali kwa usalama. Alitaja akaunti za NMB Kikundi na mpango wa Go na NMB kuwa miongoni mwa njia zinazotumiwa na benki hiyo kuwafikia wananchi, kuwajengea nidhamu ya fedha na kuwasaidia kujiendeleza kiuchumi.

Ushiriki wa NMB katika warsha hiyo ni sehemu ya juhudi za benki hiyo za kukuza elimu na ujumuishaji wa kifedha nchini, kwa kuwahamasisha Watanzania kutumia huduma rasmi za kibenki, kuweka akiba kwa malengo na kujenga msingi wa uwekezaji wa muda mrefu.