Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeendelea na juhudi za kuimarisha ushirikiano wa ulinzi wa kikanda kwa kupitia mapendekezo yanayolenga kuimarisha usalama wa pamoja, yakiwemo Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja, mafunzo ya kijeshi na ushirikiano kati ya jeshi na raia.

Mapendekezo hayo yanajadiliwa katika Mkutano wa 43 wa Baraza la Kisekta la Ushirikiano katika Masuala ya Ulinzi unaofanyika jijini Kampala, Uganda, Novemba 18, 2026, ukishirikisha Maafisa Waandamizi wa Sekta ya Ulinzi kutoka Nchi Wanachama wa EAC.

Tanzania, ikiwa ni miongoni mwa nchi waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na inayotambua umuhimu wa ulinzi, amani na usalama katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, inashiriki mkutano huo katika ngazi zote. Katika kikao cha Maafisa Waandamizi, ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Brigedia Jenerali Yohana Mrio Peter kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi.

Mkutano huo unalenga kupitia na kuoanisha mapendekezo yaliyotolewa na Kikosi Kazi cha Wataalamu wa Ulinzi kilichokutana kwa siku mbili, Novemba 16 na 17, 2026, kabla ya kuwasilishwa kwa Makatibu Wakuu na Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi kwa hatua zaidi.

Akiongoza mkutano huo, Meja Jenerali Wycliffe Keita wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) alisema majadiliano hayo ni muhimu katika kujenga msimamo wa pamoja wa Nchi Wanachama kuhusu vipaumbele vya ushirikiano wa ulinzi wa kikanda.