×

Uchunguzi Waanza, Ajali ya Mv Mwanza; Je, Ni Hitilafu ya Kiufundi au Makosa ya Uendeshaji?

Meli ya MV Mwanza inayomilikiwa na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), imegonga mwamba wa Bismarck (Bismarck Rock) katika Ziwa Victoria, wakati ikiwa safarini kutoka Bandari ya Mwanza Kusini kuelekea Mwanza Kaskazini, huku abiria wote waliokuwa ndani ya meli hiyo wakinusurika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), tukio hilo limetokea Novemba 18, 2026, majira ya saa 4:29 asubuhi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya tukio hilo, meli hiyo ilirejea salama katika Bandari ya Mwanza Kusini majira ya saa 6:12 mchana, huku abiria na watu wote waliokuwa ndani ya meli hiyo wakishuka salama.

TASAC imesema hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa kutokana na tukio hilo, na kwamba hakuna uchafuzi wa mazingira uliojitokeza.

Aidha, shirika hilo limeunda timu ya wataalamu wa uchunguzi wa ajali hiyo ambayo itaanza kazi mara moja kubaini chanzo cha tukio hilo.

TASAC imeeleza kuwa taarifa kuhusu chanzo cha ajali hiyo itatolewa kwa umma mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

 

Leave a Comment