
BOMANG’OMBE, HAI: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka vijana na wananchi kwa ujumla kuendelea kulinda amani na utulivu nchini, akisisitiza kuwa usalama ni msingi muhimu katika maandalizi ya kupokea wageni wa kimataifa watakaokuja nchini kwa ajili ya matukio mbalimbali makubwa.
Rais Samia ametoa wito huo leo, Novemba 20, 2026, alipokuwa akisalimia wananchi wa Bomang’ombe wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, akiwa njiani kuelekea mjini Moshi.
Amesema Tanzania inaendelea kuwa mwenyeji wa watalii na mikutano mbalimbali ya kimataifa, jambo alilolitaja kuwa miongoni mwa viashiria vya umuhimu wa kuendelea kudumisha amani na usalama nchini.
“Ombi langu kwenu ni amani na utulivu kwa nchi yetu,” amesema Rais Samia.

Amebainisha kuwa Tanzania inajiandaa kupokea wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali kupitia matukio makubwa yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2027, yakiwemo mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na mashindano ya urembo wa dunia.
Amesema maandalizi ya matukio hayo yanahitaji ushirikiano wa wananchi wote, hususan vijana, katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na mazingira salama na yenye utulivu kwa wageni na wananchi.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Hai kuwa Serikali imetenga tena fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko la kimataifa litakalosaidia kukuza biashara na kuboresha maisha ya wakulima.
“Ninataka niwahakikishie, tunakwenda kujenga soko la kimataifa ndani ya wilaya hii,” amesema Rais Samia.
Ameeleza kuwa soko hilo litakuwa fursa muhimu kwa wakulima kupata eneo la uhakika la kuuza mazao yao, kuongeza shughuli za biashara na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.
Rais Samia yupo mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kushiriki shughuli za kitaifa mjini Moshi, ikiwemo ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi unaofanyika katika Shule ya Polisi (CCP).
Aidha, ameahidi kurejea mkoani humo kwa ziara rasmi ya kikazi, ambapo atatembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kupata fursa ya kuzungumza na wananchi kuhusu masuala yanayohusu maendeleo yao.