
Nahodha wa zamani wa meli ya kitalii ya Costa Concordia, Francesco Schettino, ameachiwa kutoka gerezani baada ya kutumikia kifungo cha zaidi ya miaka 14 kufuatia ajali ya kuzama kwa meli hiyo iliyosababisha vifo vya watu 32 nchini Italia mwaka 2012.
Schettino, mwenye umri wa miaka 66, aliachiwa huru Ijumaa, Novemba 20, 2026, kwa amri ya Mahakama ya Uangalizi ya Roma, baada ya kupata nafuu ya muda wa kifungo kutokana na mwenendo mzuri gerezani.

Ajali hiyo ilitokea Januari 13, 2012, wakati meli ya Costa Concordia ikiwa na takribani abiria 3,200 pamoja na zaidi ya wafanyakazi 1,000 ilipogonga mwamba wa baharini karibu na Kisiwa cha Giglio katika Bahari ya Mediterania na kuanza kupinduka.
Tukio hilo lilisababisha vifo vya watu 32 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, na kuwa moja ya ajali kubwa za meli za kitalii kuwahi kutokea barani Ulaya.

Baada ya uchunguzi na kesi iliyodumu kwa takribani miezi 19, Schettino alikutwa na hatia ya kuhusika na vifo vya watu pamoja na kuitelekeza meli kabla ya abiria wote kuokolewa. Februari 2015 alihukumiwa kifungo cha miaka 16 jela.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Italia, alipata punguzo la takribani miaka miwili ya kifungo kutokana na mwenendo mzuri na utaratibu wa kisheria unaowaruhusu wafungwa kupata siku 45 za punguzo kwa kila miezi sita ya mwenendo mzuri.
Baada ya kuachiwa, Schettino atatekeleza kipindi cha uangalizi maalumu katika eneo la Campania, Italia, huku akifanya kazi katika kampuni binafsi. Pia amewekewa masharti ya kutotoka nyumbani kati ya saa nne usiku na saa kumi na mbili asubuhi.
Wakili wake, Francesca Carnicelli, amesema mteja wake amefurahishwa na nafasi hiyo aliyopewa na mahakama, lakini anatambua kuwa bado ana wajibu wa kuendelea kutekeleza masharti ya hukumu yake.
Schettino alikosolewa vikali baada ya ajali hiyo kwa madai ya kuibadilisha njia ya meli na kuisogeza karibu mno na ufukwe, kitendo kilichosababisha kugonga mwamba.
Pia alikabiliwa na lawama kwa kushindwa kutumia ipasavyo mifumo ya kisasa ya urambazaji, kuchelewa kutoa taarifa kwa mamlaka kuhusu ajali na kuondoka kwenye meli wakati abiria wengi walikuwa bado hawajaokolewa.
Kuachiwa kwake sasa, miaka 14 baada ya janga hilo, kumehitimisha sehemu ya safari yake ya kifungo, ingawa masharti ya uangalizi yanaendelea kutumika.