×

Maua Sama Aingilia Mvutano wa Zuchu na Nandy, Atoa Ujumbe Mzito

Msanii wa Bongo Fleva, Maua Sama

Msanii wa Bongo Fleva, Maua Sama, ameonekana kutoa ujumbe unaoweza kutafsiriwa kama dongo kufuatia mvutano wa maneno unaoendelea mitandaoni kati ya wasanii wenzake Zuchu na Nandy.

Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Maua Sama amesisitiza umuhimu wa wasanii kuelekeza nguvu zao katika muziki badala ya kutumia muda mwingi kurushiana maneno mitandaoni.

Msanii wa Bongo Fleva, Bongo Fleva, Zuhura Othman maarufu Zuchu.

Katika ujumbe wake ameandika:

“Sikuhizi sifungui mdomo, so siingizi shoti. TUIMBENI JAMANI… TUIMBENI tuache maneno maneno…!! The cake is too big DJ Play SIMAMA Maisha yaendelee.”

Kauli hiyo imekuja wakati ambapo Zuchu na Nandy wamekuwa wakitupiana vijembe kupitia mitandao ya kijamii, hali iliyozua mijadala miongoni mwa mashabiki wa Bongo Fleva.

Wakati mjadala huo ukiendelea, Nandy ameendelea na maandalizi ya albamu yake mpya aliyoipa jina la 911, baada ya kutangaza orodha ya nyimbo 16 zitakazopatikana ndani ya albamu hiyo inayotarajiwa kutoka Novemba 27, 2026.

Staa wa kike wa Bongo Fleva, Faustina Mfinanga almaarufu Nandy.

Nandy, ambaye jina lake halisi ni Faustina Charles Mfinanga, amesema maandalizi ya albamu hiyo yameambatana na changamoto mbalimbali zilizowahi kumfanya kufikiria kukata tamaa, lakini kwa msaada wa Mungu amefanikiwa kuikamilisha.

Ameitaja 911 kuwa albamu ya ndoto zake na mwanzo mpya katika safari yake ya muziki, huku akiwashirikisha wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya Afrika.

Katika ujumbe wake, Nandy amesema muziki umebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa na kumshukuru Mungu kwa kumwezesha kuvuka changamoto alizokutana nazo wakati wa maandalizi ya kazi hiyo.

“Mimi ni binti tu mwenye vision, uthubutu na mwenye kiu ya mafanikio, mwenye passion ya muziki, sababu najua muziki umebadilisha maisha yangu 100%, bila Mungu nisingekuwa hapa leo, yeye ndiye aliyenibeba nilipokuwa nimechoka, nilipokuwa sina nguvu tena,” ameandika Nandy.

Kwa upande mwingine, Zuchu ameendelea kuisukuma video ya wimbo wake Mvua Ya Baraka aliomshirikisha Diamond Platnumz, ambayo imeendelea kupata mwitikio kutoka kwa mashabiki tangu ilipotoka.

Hali hiyo imefanya mjadala kuhusu muziki, mafanikio na ushindani kati ya wasanii hao kuendelea kutawala mazungumzo kwenye mitandao ya kijamii, huku kila mmoja akiendelea na shughuli zake za kimuziki.

Leave a Comment