×

Simanzi India: Watu 17 Wafariki Baada ya Kunywa Pombe Yenye Sumu, 200 Walazwa Hospitalini

Watu wasiopungua 17 wamefariki dunia huku zaidi ya 200 wakilazwa hospitalini kufuatia tukio la kunywa pombe inayodaiwa kuchanganywa na kemikali yenye sumu katika jimbo la Manipur, kaskazini mashariki mwa India.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mamlaka za eneo hilo, idadi ya vifo iliongezeka kutoka 11 hadi 17 kufikia Jumapili, Novemba 22, 2026, huku juhudi za kuokoa maisha ya waathirika zikiendelea.

Waziri Mkuu wa jimbo la Manipur, Yumnam Khemchand Singh, amethibitisha kuongezeka kwa idadi ya vifo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, huku akieleza kuwa chanzo cha pombe hiyo kinahusishwa na mji wa Chakpikarong, wilayani Chandel, karibu na mpaka wa India na Myanmar.

Taarifa zilizoripotiwa na magazeti ya The Times of India na The Hindu zinaeleza kuwa watu 228 kati ya 1,130 waliofanyiwa uchunguzi kutokana na dalili za kuathirika na sumu walilazimika kulazwa katika vituo viwili vya matibabu.

 

Katika hatua nyingine, mamlaka zimewakamata watu sita wanaohusishwa na tukio hilo huku zikikamata karibu galoni 1,200 za pombe inayoshukiwa kuwa na uchafuzi kwa ajili ya uchunguzi wa maabara.

Kwa sasa, uchunguzi unaendelea kubaini chanzo halisi cha uchafuzi huo, waliohusika katika usambazaji wa pombe hiyo pamoja na ukubwa wa madhara yaliyotokana na tukio hilo.

Tukio hilo limezua tahadhari kuhusu hatari ya unywaji wa pombe zisizodhibitiwa, hasa zile zinazoweza kuchanganywa na methanol, kemikali yenye sumu kali ambayo inaweza kusababisha upofu, uharibifu wa viungo vya mwili na hata kifo.

Leave a Comment