×

Wolper Aomba Talaka kwa Rich Mitindo, Afunguka Mazito “Hakuna Tena cha Kusuluhisha”

Muigizaji na mfanyabiashara nchini, Jackline Wolper, akiwa na mume wake, Rich Mitindo siku ya ndoa yao.

Muigizaji na mfanyabiashara nchini, Jackline Wolper, amefichua kuwa amechukua hatua za kuomba talaka kutoka kwa mume wake, Rich Mitindo, baada ya kuona kuwa tofauti zilizopo katika ndoa yao haziwezi tena kutatuliwa.

Wolper amesema tayari amefikisha nyaraka zinazohusiana na talaka mahakamani, ingawa mchakato wa kisheria bado haujakamilika, huku akimtaka mume wake kushirikiana ili kila mmoja aweze kuendelea na maisha yake.

Wolper amesema amepitia changamoto mbalimbali katika maisha yake, ikiwemo matatizo ya kifedha na kimahusiano, lakini kwa sasa hana matumaini ya kurekebisha tofauti zilizopo kati yake na Rich.

Amedai kuwa jitihada mbalimbali za kusuluhisha matatizo yao hazijazaa matunda, akieleza kuwa hata vikao vilivyohusisha kanisa pamoja na wazazi havikuweza kufanikisha maridhiano.

Hata hivyo, Wolper amesisitiza kuwa hana nia ya kumsema vibaya Rich Mitindo kwa kuwa ni baba wa watoto wake na bado anamheshimu licha ya changamoto zilizowakabili katika ndoa yao.

“Richi kagoma kubadilika, kwa hiyo sitaki kumsemea kwa sababu ni baba wa watoto wangu. Sitaki kumuongelea vibaya kabisa. Lakini hakuna haja ya uhasama, kila mtu aendelee na maisha yake,” alisema Wolper.

Kuhusu suala la mali, Wolper amesema kila mmoja ana mali zake binafsi na kwamba hawakuwa na miradi mingi mikubwa waliyoianzisha kwa pamoja, isipokuwa biashara ya suti ambayo kwa sasa imesimama.

Ameeleza kuwa hana nia ya kuingia katika mgogoro wa kugawana mali, akisisitiza kuwa hatamani mali za mumewe wala hana sababu ya kuamini kuwa Rich anatamani mali zake.

Akizungumzia matarajio yake ya maisha ya baadaye, Wolper amesema anatamani kuwa na mwenza ambaye watashirikiana katika kujenga maisha, kugharamia mahitaji na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa pamoja.

Pia amefichua ndoto yake ya kuwa na nyumba katika eneo tulivu, mbali na pilikapilika za mjini, ambako angependa kuishi hadi uzeeni.

Aidha, Wolper amekiri kuwa kuna wanaume wanaomvutia na wanaotamani kuwa naye kimapenzi, lakini kwa sasa anazingatia heshima ya ndoa yake kwa kuwa bado hajapewa talaka rasmi.

“Wapo watu ambao wanani-admire na wanatamani kuwa na mimi, lakini nadhani naiweka heshima kwa sababu bado sijapewa talaka. Hata hivyo, hilo halinizuii kuendelea na maisha yangu,” alisema.

Kauli hiyo imeweka wazi msimamo wa Wolper kuhusu mustakabali wa ndoa yake na Rich Mitindo, huku akisisitiza kuwa anachotaka kwa sasa ni kumaliza mchakato wa talaka kwa amani na kuendelea na maisha, hasa katika malezi ya watoto wake na shughuli zake za kibiashara.

Leave a Comment