
DAR ES SALAAM: Jiji la Dar es Salaam linatarajiwa kuwa kitovu cha sifa, ibada na muziki wa Injili Desemba 4, 2026, wakati tamasha kubwa la Sifa Gospel Fest litakapofikia kilele chake katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama.
Tamasha hilo linalokuja baada ya safari ya kusifu, kuabudu na kueneza Injili katika maeneo mbalimbali nchini, linatarajiwa kuwakutanisha waimbaji maarufu wa muziki wa Injili pamoja na waumini kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania.
Akizungumza leo Novemba 24, 2026, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, QS Suma Mwaitenda, ametangaza orodha ya wasanii watakaohudumu katika jukwaa hilo, huku majina ya waimbaji wakubwa yakitajwa.

Miongoni mwa wasanii waliotangazwa ni Henrick Mruma, Bony Mwaitege, Rose Muhando, Elia Mtishibi, Boaz Danken, Paul Clement, Godfrey Steven, Kibonge wa Yesu na Obi Alpha, pamoja na wengine wengi.
Mbali na waimbaji hao wa kujitegemea (Solo Artists), tamasha hilo pia litashirikisha vikundi na kwaya mbalimbali za muziki wa Injili, zikiwemo Neema Gospel Choir, Kwaya ya Mtakatifu Kizito Makuburi na Agape Gospel Band.

Kuelekea kilele hicho, Sifa Gospel Fest tayari imepita katika mikoa ya Mbeya, Geita, Mwanza, Arusha na Dodoma, ambako waumini walipata nafasi ya kushiriki katika ibada za sifa na kuabudu pamoja na kusikiliza ujumbe wa Injili.
Desemba 4, macho na masikio ya mashabiki wa muziki wa Injili yataelekezwa viwanja vya Posta, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kushiriki tukio hilo linalolenga kuunganisha watu kupitia muziki, sifa na ibada.
Sifa Gospel Fest si tukio la burudani pekee, bali ni mwaliko kwa watu wa rika na makundi mbalimbali kukutana katika uwepo wa Mungu, kuinua sauti zao na kumtukuza Muumba.
