×

Yanga Yawapa Wananchi Silaha ya Kuivamia MC Alger Zanzibar

Klabu ya Yanga imewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi na kukata tiketi mapema kwa ajili ya mchezo dhidi ya MC Alger wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaochezwa visiwani Zanzibar.

Hatua hiyo imekuja baada ya klabu hiyo kuingia makubaliano na kampuni ya Lipa Tiketi kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa tiketi kupitia mfumo wa kidijitali unaomwezesha shabiki kununua tiketi kwa kutumia simu janja au simu za kawaida.

Kupitia mfumo huo, shabiki anayetaka kununua tiketi anatakiwa kubonyeza _149_46\*11# na kufuata maelekezo, huku wengine wakitumia tovuti ya Lipa Yanga kupitia anuani ya http://yanga.lipatickets.tz/.

Akizungumza kuhusu mfumo huo, mwakilishi wa Lipa Tiketi, Fahad Habib, amesema wamefurahi kuaminiwa na Yanga, akieleza kuwa mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa tiketi, kudhibiti ubora wa mauzo na kusaidia ukusanyaji wa kodi.

Amesema mfumo huo unapatikana kwa watumiaji wa simu zote na kuwataka mashabiki kuanza kuutumia katika mchezo huo dhidi ya MC Alger.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa Yanga, Alikamwe, shabiki mmoja anaweza kununua hadi tiketi nne kupitia mfumo huo, huku utaratibu maalumu ukiandaliwa kwa wale wanaohitaji kununua tiketi nyingi zaidi.

Alikamwe amesisitiza kuwa mashabiki wanapaswa kuelewa kuwa jukumu la kuipa Yanga ushindi si la wachezaji pekee, bali pia ni la mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi na kujaza uwanja.

Amesema ili timu iweze kufanya vizuri katika michezo yake ya nyumbani, ni muhimu mashabiki kuhakikisha wanapata tiketi mapema na kutoa sapoti kwa wachezaji.

“Tunaposema tunakwenda kuwabonda hawa Waarabu, jambo la kwanza ni kuhakikisha tunawabonda kwa kukata tiketi na kujaza uwanja. Tukishafanya hivyo, basi kazi inayofuata ni kwenda kuwabonda ndani ya dakika 90 za mchezo,” amesema Alikamwe.

Wakati huohuo, kikosi cha wachezaji 30 wa Yanga kimeondoka kuelekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya maandalizi ya mchezo huo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga sasa inatarajia kutumia nguvu ya mashabiki wake kama sehemu ya maandalizi ya mchezo huo, huku ikiwataka Wananchi kujitokeza kwa wingi na kuifanya Zanzibar kuwa na shamrashamra za kijani na njano.

Viingilio vya mchezo huo vitakuwa kama ifuatavyo:
Jukwaa la Saa na Obit – Tsh 5,000
Jukwaa la Urusi – Tsh 10,000
Wings (pande zote mbili) – Tsh 20,000
VIP – Tsh 30,000

Leave a Comment