×

Rais Samia Amzawadia Mkubwa Fella Gari la Toyota Vellfire

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemzawadia mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Said Hassan Mlinge maarufu kama Mkubwa Fella, gari aina ya Toyota Vellfire kwa lengo la kumsaidia katika changamoto za usafiri, hususan safari za hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Gari hilo limekabidhiwa Ijumaa, Novemba 27, 2026, jijini Dar es Salaam kupitia kwa msanii Chege Chigunda na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Mitandaoni Tanzania (JUMIKITA), Shaban Matwebe.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Matwebe amemshukuru Rais Samia kwa kumjali na kumsaidia Mkubwa Fella, akieleza kuwa zawadi hiyo itakuwa msaada mkubwa katika kipindi hiki ambacho mkongwe huyo anakabiliwa na changamoto za kiafya.

Amesema gari hilo litapunguza usumbufu wa usafiri, hasa wakati wa kwenda hospitalini kwa ajili ya matibabu na kliniki, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kumuunga mkono katika kipindi anachopitia.

Zawadi hiyo imekuja ikiwa imesalia siku mbili kabla ya kufanyika kwa hafla maalumu ya **Heshima kwa Mkubwa**, inayotarajiwa kufanyika Novemba 29, 2026, katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, kuanzia saa sita mchana.

Hafla hiyo iliyoandaliwa na JUMIKITA kwa kushirikiana na wadau wa muziki inalenga kumuenzi Mkubwa Fella akiwa hai na kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo na ukuaji wa muziki wa Bongo Fleva nchini.

Aidha, tukio hilo litakuwa sehemu ya kuhamasisha ukusanyaji wa michango kwa ajili ya kumsaidia katika matibabu na mahitaji yake, huku likitarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, wasanii pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya sanaa.

Hatua ya Rais Samia kumzawadia gari Mkubwa Fella imeongeza ishara ya mshikamano na kuthamini mchango wa mkongwe huyo katika tasnia ya muziki, ambaye kwa miaka mingi amekuwa sehemu ya safari na maendeleo ya Bongo Fleva nchini Tanzania.

Leave a Comment