The House of Favourite Newspapers

Vodacom Yachangia Milioni 10 Kuwasaidia Wafiwa Ajali Ya MV Nyerere

Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom kupitia taasisi yake ya Vodacom Foundation imetoa Sh10 milioni ili zitumiwe na wafiwa katika maziko ya ndugu na jamaa zao waliopoteza maisha katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama juzi Septemba 20, 2018.

Fedha hizo zimekabidhiwa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mwasiliano, Isack Kamwelwe na meneja wa Vodacom Kanda ya Ziwa, Domisian Mkama.

Hafla ya makabidhiano hayo yamefanyika katika kijiji cha Bwisya kisiwa cha Ukara leo Jumamosi Septemba 22, 2018.

“Awali tulipanga kutengeneza majeneza 100 lakini tumeona ni vyema kukabidhi fedha kwa Serikali ili isimamie kutengeneza na kugawa majeneza kwa waliopoteza ndugu zao katika ajali hii,” amesema Mkama.

Baada ya kupokea fedha hizo, Waziri Kamwelwe naye alizikabidhi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama ambaye pia alizikabidhi kwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.
Mhagama aliagiza ifunguliwe akaunti maalum na mkoa huo kwa ajili ya kuhifadhi fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa ajali hiyo.

Comments are closed.