×

Wananchi Wapanga Kutoa Sadaka Kisa Maji, Mbarawa Awatoa Hofu

Tatizo la maji lililokuwa likiwakabili wananchi wa wilayani Moshi mkoani kilimanjaro, linatarajiwa kupatiwa ufumbuzi hivi karibuni, baada ya serikali kutenga Sh. 500 Milioni, kwa ajili ya kutekeleza Mradi mkubwa wa Maji kutoka ziwa Chala.

 

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa amesema hayo wakati akikagua mradi wa maji katika kijiji cha Mdawi kata ya Kimochi Wilaya ya Moshi, unaotekekezwa na mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira Mjini Moshi (Muwsa) kwa gharama ya ya zaidi ya Shilingi milioni 100, ambapo amesema kuwa serikali imejipanga kukabiliana na tatizo la maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini yenye uhaba wa maji safi na salama.

 

Amesema kuwa fedha hizo zitatolewa na serikali mwezi huu wa Machi 2020, ili kuhakikisha mradi huo unaanza mara moja na wananchi wanaondokana na kero kubwa ya maji ambayo imewakabili kwa muda mrefu.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa, Aron Joseph, amesema Mradi wa Maji katika Kijiji cha Mdawi, utakaogharimu zaidi ya Sh 100 milioni,umekamilika kwa asilimia 95 na utawanufaisha zaidi ya Wakazi 3000 wa kijiji hicho.

 

Naye Mtendaji wa Kijiji cha Mdawi Lazaro Paul na wananchi wa kijiji hicho, wamesema maji yamekuwa ni kero kubwa katika kijiji hicho, hali ambayo iliwalazimu kununua maji dumu moja la lita 20 kwa Sh 500.

Leave a Comment