
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemnyang’anya Waziri Mkuu mstaafu, Mhe. Frederick Sumaye shamba lake lenye ukubwa wa hekta 33 baada ya kushindwa kuliendeleza.
Akitoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema Serikali imefikia uamuzi huo baada ya Sumaye kushindwa kuliendeleza kama notisi ya siku 90 ilivyoeleza.
“Oktoba 28, mwaka huu, Rais John Magufuli alibatilisha hati ya kumiliki ardhi ya shamba namba 3074 lililopo Mabwepande. Shamba hili lilikuwa na hati namba 53086. Jina la mmiliki lililoandikwa katika hati ni Frankline Sumaye,” amesema DC Hapi.
Sumaye ambaye alikuwa ni mmoja wa wasemaji tegemeo katika mikutano ya kampeni ya Uchaguzi Mkuu uliopita ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anamiliki mashamba makubwa yaliyoko Morogoro na Mabwepande Dar es Salaam.
Baada ya Rais Magufuli kubatilisha hati hiyo, Hapi amesema kuanzia sasa ni marufuku kwa Sumaye kujihusisha na shamba hilo maana hati yake imeshabatilishwa na akibainika kufanya chochote vyombo vya dola vitachukua nafasi yake.
