×

Tammy: Mwaka Mmoja Ujao Nitakuwa Anga Zingine

Stori: OJUKU ABRAHAM | RISASI MCHANGANYIKO | DAR ES SALAAM

TAMARAH Ally Nyamgunda ni binti mdogo tu aliyezaliwa Februari 14, 1992 jijini Dar es Salaam, lakini miaka 25 baadaye, jamii inamtambua kama The Baddest, rapa wa kike anayetamba na kibao cha Mtoto wa Kike, akisimamiwa na Mziki Mnene Entertainment.

Anaonekana mgeni katika Hip Hop, lakini ukweli ni kwamba ameanza siku nyingi harakati za kutafuta tobo la kutokea katika maisha.

Baada ya kumaliza kidato cha sita mwaka 2011 pale Jitegemee Sekondari, mwishoni mwa mwaka huo akajiunga na Lebo ya Young Chall’s iliyopo MJ Records, ikisimamiwa na mtayarishaji mahiri, Marco Chali.

Akiwa pamoja na rapa mwingine mkali lakini mdogo, Chemical katika kundi hilo, walifanikiwa kufanya wimbo uliokuja kumtangaza uitwao Dezodezo, ambao walimshirikisha Tunda Man.

Miaka mitatu baadaye akajitoa kundini na kubakia kivyake, ambapo alifanya ngoma na rapa wa kiume, Beka Tittle pamoja na G Nako ulioitwa Down Low.

Hadi sasa, Baddest ameshafanya shoo tano, ambazo kwake ni dalili njema kuelekea kwenye mafanikio, kwa sababu mwanga unaonekana.

“Nimehaso sana katika kutafuta haya maisha, kuna kipindi nililazimika kupumzika kidogo kutokana na matatizo ya kifamilia, lakini sasa nimerudi kwa ajili ya kutimiza ndoto zangu,” anasema rapa huyo aliyevutiwa na aina hiyo ya muziki kutoka kwa Fox Brown wa Marekani.

Juu ya kwa nini amechagua rap, muziki ambao unaonekana mgumu na usiouzika, hasa kwa watoto wa kike, Baddest anakanusha kuhusu kutouza kwa aina hiyo ya muziki, akisema inategemea nini msanii anaimba na namna anavyojiweka.

“Siyo kweli kwamba Hip Hop haiuzi, inategemea na msanii mwenyewe na jinsi anavyojiweka, mimi napenda ku-rap, siwezi kuimba maana ile misingi ya uimbaji sijawahi kuifuata, naamini naweza kufanya vizuri kwenye huu muziki, hilo nina uhakika nalo,” anasema Baddest.

Wakati akikua na damu yake kuzama katika muziki, alipenda namna Dattaz, yule rapa mkongwe wa kike aliyepata kuvuma na kibao chake cha Mume wa Mtu, jinsi alivyokuwa akifanya muziki wake.

Lakini siku ya kwanza kukutana naye, akiamini ni hatua kubwa kwake, alikutana na kitu cha ajabu: “Mimi ni shabiki mkubwa sana wa muziki wa Dattaz, siku hiyo nilipokutana naye nilifurahi sana, naye alipatwa na furaha sana vilevile, lakini nilishangaa sana nilipomuambia na mimi nafanya muziki, ghafla furaha yake ikaondoka, kwa kweli jambo lile lilinisononesha sana.”

Swali: Muziki una hatua nyingi mnapitia, ukiachana na hela, kuna rushwa ya ngono pia, kwako umekutana nayo hii?

Baddest: Nimekutana nayo sana lakini nilifanikiwa kuikwepa, huwa sishughuliki na mtu mwenye dalili za kunitamani.

Swali: Muziki umekufanya ufahamiane na wasanii wakubwa, unajisikiaje?

Baddest: Ninajisikia vizuri sana hasa jinsi walivyonipokea, kwangu ni kitu kikubwa sana, nashukuru kila mtu ana furaha na Tammy.

Swali: Nini malengo yako?

Baddest: Nataka niwe msanii mkubwa, mkubwa kama Diamond au Vanessa au Yemi Alade, ninaona dalili kwa sababu sasa hivi ninapata coverage hadi MTV, mwaka mmoja ujao nitakuwa mbali sana.

Swali: Nini ushauri wako kwa wasanii wenzako?

Baddest: Wasanii waache ubinafsi, nilikuwa Nigeria, wanashangaa sana jinsi tunavyochukiana, wenzetu kule wanapendana sana, kila kitu ni Nigeria kwanza, lakini sisi tunapigana sana vita, tunaonekana hatuna upendo.

Swali: Rushwa katika muziki unaizungumziaje?

Baddest: Siyo tu katika muziki, rushwa ni tatizo Afrika nzima, kule Nigeria ndiyo balaa, nimeshuka pale uwanjani kila mtu anataka hela.

Baddest au Tammy ni dada wa hiyari wa mchezaji nyota wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars na Mwadui ya Shinyanga, Hassan Kabunda, mtoto wa beki wa zamani wa Yanga, Salum Kabunda ‘Ninja’.

Leave a Comment