RWANDA: Serikali ya Rwanda imetangaza tarehe za kufanya uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika mwakani 2017.
Kulingana na tangazo lililotolewa baada ya kikao cha baraza la mawaziri, uchaguzi huo utafanyika Agosti 4, 2017 huku kampeni zikitarajiwa kuanza mwezi Julai lakini hakuna tarehe rasmi iliyotangazwa kwa wagombea kuwasilisha hati za kugombea urais, licha ya kwamba tangazo hilo linasema wagombea watatangazwa kabla ya kuanza kwa kampeni.
Kwa mujibu wa katiba mpya, Rais Paul Kagame (pichani chini) anaruhusiwa kuwania muhula wa tatu.
Mtu pekee katika kambi ya upinzani aliyetangaza nia yake ya kugombea urais ni kasisi wa zamani wa Katoliki, Joseph Nahimana.
Hata hivyo juhudi zake za kutaka kurejea nchini Rwanda wiki mbili zilizopita ili kuandikisha chama chake na kugombea urais ziligonga mwamba.
Kasisi Joseph Nahimana na wenzake watatu walikataliwa kuingia nchini Rwanda walipokuwa mjini Nairobi Kenya kuelekea Rwanda kutoka nchini Ufaransa anakoishi kama mkimbizi.


