Q Jay.
Na Hashim Aziz | Gazeti la Ijumaa, Toleo la Jan. 06, 2017
Q Jay ama ukipenda waweza muita Joseph Kelvin Mapunda. Ni mmoja kati ya wasanii wa RnB Bongo waliowahi kutikisa vilivyo akiwa na kundi lake la Wakali Kwanza lililokuwa likiundwa na Makamua na Joslin.
Nani ambaye hakumbuki au hatambui kipaji kikubwa cha kuimba alichokuwa nacho Q Jay? Nani atabisha kwamba bado hajapatikana msanii mwenye sauti na melody kali kama Q Jay? Lakini nini kimemsibu? Yako wapi yale mashairi yake matamu? Ipo wapi ile sauti yake yenye mvuto wa kipekee? Kila kitu kimeyeyuka, kama theluji iyeyukavyo juani.
Ni simulizi ya kusikitisha lakini ni lazima isimuliwe pengine inaweza kuwa dawa kwa Q Jay mwenyewe na watu wengine wenye tatizo kama lake! Pengine inaweza kuwa dawa ya kumrudisha mkongwe huyu kwenye gemu kwa sababu naamini bado anacho kipaji cha hali ya juu na mashabiki wanamhitaji.
Q Jay na D Malick
Hivi karibuni, Q Jay alitembelea kwenye ofisi za gazeti hili akiongozana na mkali mwingine, D Malick wanayeunda naye kundi jipya la Busy Boys Chatterd kwa ajili ya mahojiano na Global TV Online.
Kwa wafuatiliaji wa masuala ya muziki, watakumbuka kwamba mkali huyu aliyewahi kuwika na vibao vingi ikiwemo Sifai, aliwahi kutangaza kuachanana muziki wa kidunia na kuimba Gospel.
Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu, taarifa zikaanza kuzagaa kwamba Q Jay amekuwa akionekana kwenye kumbi za starehe, akiwa amepiga mitungi hatari! Ikawa inafika muda mchizi analewa mpaka hajielewi. Hakuna aliyekuwa na majibu ya nini kilichotokea.
Katika makala haya yanachambua historia yake ya kusikitisha iliyotokea na kusababisha kupotea katika muziki.
Showbiz: Kwa kipindi kirefu Q Jay umepotea kwenye muziki, nini tatizo?
(anasita kujibu, D Malick anamuomba ruhusa amjibie)
D Malick: “Q Jay ana matatizo makubwa na mke wake na hiyo ndiyo sababu kubwa ya kupotea kwake kimuziki. Ni kweli alikuwa akilewa lakini sasa hivi namshukuru Mungu ameanza kutulia kiakili ingawa siyo sana.
“Alikuwa hataki kusema matatizo yake japo alikuwa na hali mbaya sana. Kuna kipindi ilifika hata akikaa mwenyewe analia tu, ukimuuliza nini kinakuliza anakosa majibu. Alimpenda sana mkewe lakini akaja kumuumiza vibaya. Tunatakiwa kumsapoti ili aweze kurudi kwenye hali yake kama zamani,” alisema D Malick na kuamsha mjada.
Q Jay alipoulizwa kama alichosema D Malick ni kweli, alikubali japokuwa alikuwa mgumu wa kufunguka kila kitu. Baada ya kubanwa sana, alifunguka kwamba, yeye na mkewe (jina linahifadhiwa), walibahatika kupata watoto wanne lakini baadaye, alikuja kugundua kwamba eti mtoto wao wa kwanza, hakuwa damu yake!
Akasema kuwa mkewe alimchezea faulo, akabeba ujauzito wa mtu mwingine wakati akiwa naye, akamuaminisha kwamba mtoto alikuwa ni wake hadi anafikisha miaka sita.
Q Jay: “Baada ya kugundua hayo, kwa jinsi nilivyokuwa nampenda mke wangu, nilichanganyikiwa nikahisi dunia imefika mwisho. Mpaka sasa huwa nikikaa na kufikiria, machozi yananitoka mwenyewe. Niliamua kuokoka kama njia ya kutafuta sehemu ya kutua maumivu niliyokuwa nayo lakini bado niliona nazidi kuteseka,” anasema msanii huyo.
Q Jay amefunguka mengi, mapitio yake yote yalivyokuwa. Ili kuipata exclusive interview tembelea Global TV kupitia www.globaltvtz.com