
Shinikizo la juu la damu (presha) hutokea pale moyo unapodunda na kusukuma damu nyingi lakini damu hiyo ikashindwa kusambaa kwa kasi kwenda kwenye viungo vingine vya mwili kutokana na wembamba wa mishipa ya damu.
Hali hii husababisha mishipa ya damu kupasuka, viungo vya ndani ya mwili kuharibika na wakati mwingine husababisha moyo kusimama ghafla na mtu kupoteza maisha.
Zipo sababu nyingi zinazosababisha mishipa ya damu kuwa myembamba lakini kubwa ni kurundikana kwa mafuta kwenye kuta za mishipa hiyo, jambo linalosababisha ishindwe kupitisha damu vizuri.
DALILI ZA PRESHA
Utafiti unaonesha kwamba watu wengi huugua ugonjwa wa presha kwa muda mrefu lakini hakuna dalili zozote zinazoonekana mpaka tatizo linapokuwa kubwa. Zipo dalili chache ambazo hata hivyo, huwatokea baadhi ya watu tu zikiwemo kutokwa na damu puani mara kwa mara na kusikia kizunguzungu.
Wengi huanza kuona dalili wakati tatizo limeshakuwa kubwa na hivyo kushindwa kulipatia tiba ya kudumu.
Njia pekee inayoweza kukurahisishia kujua kama una tatizo la presha ya kupanda, ni kwenda hospitali kupima mara kwa mara. Kwa kawaida, binadamu ambaye hana tatizo lolote la moyo, majibu ya mapigo ya moyo hutakiwa kuwa 120/80mmHg, endapo majibu yako yataonesha kuwa juu au chini ya kiwango hicho, ni dalili kwamba unaugua presha.
Hatari ya kupata presha huongezeka kadiri umri unavyokwenda na jinsi mwili wako ulivyo. Watu wanene huwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa huu.
NINI HUSABABISHA UGONJWA HUU
Sababu zinazoweza kumfanya mtu apate ugonjwa huu wa shinikizo la juu na damu, zipo nyingi lakini zinatokana na mfumo wa maisha ya kila siku, huku watu weusi wakitajwa kuwa kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa huu ukilinganisha na Wazungu.
Sababu hizo ni uvutaji sana wa sigara, unywaji wa pombe wa kupitiliza, kutoushughulisha mwili na matokeo yake kunenepeana (obesity), matatizo ya figo, ugonjwa wa Kisukari, matumizi ya madawa ya kulevya hasa Cocaine na Amphetamine na tatizo la kukosa usingizi.
Sababu nyingine ni kuwa na msongo wa mawazo, umri mkubwa, matumizi ya baadhi ya dawa za uzazi wa mpango kwa wanawake, kutofanya mazoezi, kuwa na mazoea ya kuweka chumvi nyingi kwenye chakula na matatizo ya kurithi.
NAMNA YA KUJIKINGA
Wataalamu wa masuala ya afya, wanaeleza kwamba njia nyepesi zaidi ya kuzuia usipatwe na ugonjwa huu, ni kufanya mazoezi angalau kwa nusu saa kila siku, kuwa na mtindo mzuri wa maisha kwa kula chakula bora, kutokunywa pombe kupitiliza, kuacha uvutaji wa sigara na kupata muda wa kutosha wa kupumzika.
Njia nyingine ni kuepuka kukaa na msongo wa mawazo, kutotumia dawa kiholela mpaka upate maelekezo ya daktari, kuepuka matumizi ya madawa ya kulevya na kutotumia chumvi nyingi kwenye chakula.