
MAMIA ya wasomaji wa magazeti ya Global Publishers mwanzoni mwa wiki hii walijichanganya vilivyo katika kujaza na kutuma kuponi za shindano la awamu ya pili ya Shinda Nyumba iliyozinduliwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam. Uchangamfu huo unatokana na ukweli kuwa droo ndogo ya kwanza ya shindano hilo itachezeshwa Februari 8 mwaka huu ambayo washindi kadhaa wataondoka wakiwa wamejipatia pikipiki, televisheni, simu aina ya smartphone na vyombo vya ndani.
Wasomaji wakijaza kuponi za Shinda Nyumba.
Katika eneo la Kunduchi Mbuyuni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, vijana waendesha bodaboda na wauzaji wa bidhaa ndogondogo ambao walikutwa wakinunua na kujaza kuponi za shinda nyumba, walisema safari hii wamehamasika kushiriki shindano hilo la Shinda Nyumba kutokana na mafanikio ya awamu iliyopita.
Sam Kipisi, ambaye alidai ni mwendesha bodaboda wa eneo hilo, alisema tofauti na awamu iliyopita, awamu hii atajitahidi kununua magazeti mengi zaidi ili aweze kujiweka katika nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi, achilia mbali kupata habari motomoto za mastaa, kijamii na michezo.
Ofisa Promosheni wa Global Publishers, Jimmy Haroub akimsaidia msomaji kujaza kuponi ya Shinda Nyumba.
“Uzuri wa shindano hili ni kwamba kwanza unanunua gazeti unalolipenda ili kusoma habari unazozipenda, maana ukisema habari za mastaa waKibongo, habari za Kijamii na Michezo, basi unamaanisha magazeti ya Global Publishers, lakini pia kwa kupata kuponi za shinda nyumba, maana yake unapata habari nzuri halafu unajiweka pazuri kushinda nyumba au zawadi nyingine,” alisema Sam.
Wakazi wa Goba ambao pia walitembelewa na timu ya Shinda Nyumba, nao walisema hawawezi kukaa kimya bila kupata kuponi za shindano hilo wakati kila mmoja hivi sasa anazungumzia kuhusu zawadi bwerere kutoka Global Publishers. “Siyo lazima mtu ushinde nyumba maana hiyo ni zali la mentali kweli, lakini jamani hivi vitu kama simu na vyombo vya nyumbani uvikose?
Mimi natamani sana simu ya tachi, nitajaza kuponi hadi nipate,” alisema Consolata Simon, aliyekutwa kijiweni kwake kwa mama ntilie, huko Goba. Msomaji mwingine Unaris Yunus wa Goba njia panda, alisema awamu ya kwanza ya Shinda Nyumba hakuweza kupata zawadi yoyote, lakini safari hii moyo wake unamsukuma kuamini atakuwa miongoni mwa washindi.
Msomaji akionesha kuponi yake baada ya kuijaza na kuikata kwenye gazeti la Uwazi.
“Kwanza nasikia zawadi zimeongezeka, sasa kama mnavyosema pikipiki itatolewa kila mwezi, sasa nikose nyumba sawa, basi pikipiki, televisheni, simu, mashuka, branketi hadi vyombo vya ndani nikose, aaah jamani, Mungu nisaidie,” alisema Yunus. Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdalah Mrisho alizidi kuwasisitiza wasomaji kuhakikisha wanakata kuponi za kutosha tayari kwa droo ndogo ya kwanza ambayo itafanyika hiyo Februari 8 mwaka huu.
“Utaratibu wetu wa kutuma kuponi ni uleule, baada ya kununua gazeti letu lolote kati ya Championi, Risasi, Uwazi, Amani, Ijumaa na Ijumaa Wikienda, kata kuponi kisha jaza kwa kadiri ilivyoelekezwa, halafu peleka kwa wakala yeyote aliye jirani na wewe, maana mawakala wetu wapo nchi nzima, au kwa wale wa Dar es Salaam, wanaweza kuzileta katika ofisi zetu zilizopo Bamaga, Mwenge jijini Dar,” alisema.