
Na HAMIDA HASSAN NA GLADNESS MALLYA| IJUMAA WIKIENDA| HABARI
DAR ES SALAAM: Baada ya habari kujaa tele kwenye Wikienda kuwa shoo anazoratibu Rashida Wanjara kwenye klabu za starehe za usiku jijini Dar, huwa zinajaa mastaa wa kike kwa sababu huwaunganisha na mapedeshee wa mjini, Miss Mara huyo wa zamani amefunguka juu ya skendo hiyo.
Akizungumza na Wikienda , Rashida alisema kuwa, habari hizo si za kweli na kwamba yeye ni staa wa kitambo na amekuwa na uhusiano mzuri na mastaa wenzake ndiyo maana akiwaita kwenye shoo zake hizo almaarufu Msambwanda (zinazohusisha wanawake wenye makalio makubwa), huwa wanaitikia kwa wingi lakini si vinginevyo.
“Watu wanapenda kuzusha mambo ya ajabuajabu. Kiukweli mimi huwa ni mtu wa watu na sikosi kwenye shughuli zao hivyo ni lazima na wao wanisapoti. Hayo mambo ya kuwaunganisha na mapedeshee ndiyo nayasikia,” alisema Rashida.
Hata hivyo, Rashida alipobanwa kuwa shoo zake zimekuwa zikihudhuriwa na wanaume wenye fedha zao ambao hufika pale kwa ajili ya kuchagua msanii wanayemhitaji, alidai kuwa wanaume wengi hufika kwenye shoo hizo kwa sababu ni mbunifu ambaye amekuwa akibuni vitu vya kuwavuta watu.
“Jamani hata nyota nayo inachangia, nimekuwa nikibuni vitu vya kuwavuta watu wa jinsi zote ndiyo maana huwa wanajaa lakini hayo mengineyo ni mambo ya uongo,” alisema Rashida.
Mwisho alifunguka kuwa, anaomba watu wasimchafue kwani kazi hiyo hajawahi kuifanya na wala hatarajii.