
MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers, na Mhamasishaji Mashuhuri Afrika Mashariki na Kati, Eric James Shigongo amesea kuwa, iwapo mtu anataka kufanikiwa lazima aachane na marafiki wasiofaa katika maisha yake.

Shigongo ameyasema hayo leo Feb. 24, 2017 wakati akitoa somo kwa Watanzania kuhusu namna ya kufanikiwa katika maisha, somo alilowafundisha akiwa kwenye ofisi za Global Publishers na kurushwa LIVE kupitia YouTube channel ya GLOBAL TV ONLINE.

Katika somo hilo lenye mada ya ‘Jinsi ya kuamka upya na kuanza vizuri baada ya kuanguka’, Shigongo amesema marafiki wasiofaa siku zote wanaweza kukushauri kufanya mambo mabaya na mwisho wa siku ukaishia kwenye matataizo na usifanikiwe, ili kuepukana na hilo, ameshauri kuachana na marafiki hao na kuanzisha uhusiano / urafiki na watu wenye tija katika maisha.

Mbali na hayo, Shigongo amefundisha kuwa haijalishi mtu ana elimu kiasi gani ama hana elimu kabisa, lakini jambo la msingi kukazana kufanya mambo ya tofauti kwa nguvu zako na maarifa yako yote, ipo siku atafanikiwa na mambo yake yatakuwa mazuri.

Aidha Shigongo amewaasa Watanzania kutokukata tamaa kwenye suala la kutafuta mafanikio kwani hata yeye alipitia maisha ya umaskini lakini hakukata tamaa, aliendelea kupambana licha ya kudharauliwa na kudhihakiwa lakini mwisho wa siku akafanikiwa.

Ni mambo mengi ambayo Eric Shigongo ameyafundisha leo na atakuwa akifundisha kila JUMAA kupitia Global TV Online, LIVE saa 10:00 jioni.
TAZAMA VIDEO YA MAFUNDISHO YA MHAMASISHAJI ERIC JAMES SHIGONGO
PICHA NA DENIS MTIMA GLOBAL TV ONLINE