
Wilbert Molandi na Omari Mdose | CHAMPIONI JUMAMOSI| Dar es Salaam
SIMBA imekomaa na imekataa kabisa kufungwa na Yanga leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakisema wanataka ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Simba imesema haitaki kuiona Yanga ikitwaa ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya tatu mfululizo.
Klabu hiyo inaamini ikishinda itakuwa katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa. Mechi hii inachezwa huku timu hizo zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Oktoba Mosi, mwaka jana uwanjani hapo. Katika sare hiyo, Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 26 kupitia kwa Amissi Tambwe, huku mashabiki wa Yanga wakiamini timu yao itaibuka na ushindi, Shiza Kichuya aliisawazishia Simba dakika ya 87 kwa kona iliyotinga wavuni moja kwa moja.
Sasa kueleka mchezo wa leo utakaochezeshwa na mwamuzi Mathew Akrama, Simba iliweka kambi visiwani Zanzibar na kurejea jana mchana jijini Dar es Salaam kwa ndege huku Yanga wakiweka kambi yao Kigamboni, Dar es Salaam.
Katika msimamo wa ligi kuu, Simba ipo kileleni na pointi 51 katika mechi 22 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 49 baada ya kucheza mechi 21.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Kocha wa Simba, Joseph Omog ambaye anaiongoza timu yake kwa mara ya tatu huku mara mbili ikiwa katika ligi kuu, alisema amekiandaa kikosi chake kushinda ili kufikia malengo yake ya kutwaa ubingwa. “Hii si mechi nyepesi, hivyo tunatakiwa kuongeza umakini, tunatakiwa kutumia vema kila nafasi tutakayoipata kwa ajili ya kufunga mabao, hatutakiwi kuruhusu mashambulizi kwetu.
“Sitaruhusu mpira uchezwe langoni kwetu ili kuhakikisha tunashinda mechi hii, kwa nafasi tuliyopo katika ligi, hatutakubali kupoteza mechi yoyote kwani itatutibulia hesabu zetu,” alisema Omog raia wa Cameroon.
LWANDAMINA ATEMA CHECHE
Kocha wa Yanga, George Lwandamina ambaye anaiongoza timu yake kwa mara ya pili huku ikiwa ya kwanza katika ligi kuu, alisema: “Maandalizi kwa jumla yapo vizuri na tumejipanga kuhakikisha tunaibuka na ushindi katika mchezo huu.
“Nimewaandaa vijana wangu kwa ajili ya kufanya kazi hiyo kwa sababu tunahitaji kuwa mabingwa msimu huu na ili tuwe mabingwa ni lazima tushinde mechi hii dhidi ya Simba.” Lwandamina alisisitiza kwamba, kama timu yake ikiifunga Simba itakuwa imejiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wake kwa mara ya tatu mfululizo. “Wachezaji wangu nimewaeleza hilo na wanatambua wajibu wao,” alisema Lwandamina.
OMOG 3, LWANDAMINA 2
Hii ni mara ya tatu kwa Omog kuingoza Simba dhidi ya Yanga, huko nyuma amekaa katika benchi mara mbili ambapo moja ni katika ligi kuu na ya pili ni kwenye Kombe la Mapinduzi. Oktoba Mosi, mwaka jana Omog aliiongoza Simba kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga uwanjani hapo na Januari 11, mwaka huu aliiwezesha Simba kushinda kwa penalti 4-2 katika Kombe la Mapinduzi.
Lwandamina raia wa Zambia, hii ni mara yake ya pili kuiongoza Yanga kwani Januari 11, mwaka huu katika Kombe la Mapinduzi timu yake ilifungwa kwa penalti 4-2 yeye akiwa kwenye benchi. Hii ni mara ya 83 kwa Simba na Yanga kukutana ambapo Yanga imeshinda mechi 31, Simba 24 na kutoka sare 28. Yanga imefunga mabao 92 na Simba inayo 78.