
OFISI ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu imesema inakusudia kukabiliana na ukuzaji ujuzi ili kufikia sera ya kukuza viwanda na kujenga uchumi wa kati ili kuwezesha nguvu kazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi ili kudumisha ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ajira wa ofisi hiyo, amesema utekelezaji wa mradi huo ni hatua za makusudi za serikali kukabiliana na kiwango kidogo cha ujuzi miongoni mwa watanzania.
Alisema utafiti wa nguvu kazi uliofanyika mwaka 2014, ulionyesha idadi ya watu walioajiriwa au kuajiri katika sekta mbalimbali kuwa 20, 030,139 ambao ni sawa na asilimia 89.7 ya nguvu kazi.

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ajira wa ofisi hiyo, Robert Masatu akizungumza na wanahabari (hawapo pichani). Pembeni yake ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa ofisi hiyo, Ridhiwan Wema.
Alieleza, kiwango cha nguvu kazi cha walioajiriwa au kuajiri kinaonyesha kwamba asilimia 79.9 ya nguvu kazi ina kiwango cha ujuzi wa kati na asilimia 16.6 ya nguvu kazi ina kiwango cha juu ya ujuzi.
“Kiwango cha ujuzi nchini kipo chini ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika kuwezesha nchi kufikia uchumi wa kipato cha kati ambacho ni asilimia 12 kwa kiwango cha juu cha ujuzi, asilimia 34 kwa ujuzi wa kiwango cha kati ni asilimia 54 kwa kiwango cha ujuzi wa chini.
Hivyo serikali imejipanga kuendelea kukamilisha miongozo ya ukuzaji ujuzi kwa njia mbalimbali itakayowezesha wadau kushiriki katika utekelezaji wa mikakati ya kukuza ujuzi nchini ili kufikia sera ya kukuza viwanda na kujenga uchumi wa kati.
NA DENIS MTIMA/GPL