×

Tiba Sahihi Waathirika wa Madawa ya Kulevya!

WAKATI serikali ikipambana kwa nguvu zote kuhakikisha inadhibiti uingizaji na usafirishaji wa madawa ya kulevya nchini, Kituo cha Changamoto ni Matumaini, kimetajwa kuwa miongoni mwa vituo vinavyotoa tiba sahihi kwa waliothirika na madawa hayo.

Kituo hicho kilichopo Boko Magengeni barabara ya kuelekea Bagamoyo, jijini Dar kilianzishwa mwaka 2007, mpaka sasa kimefanikiwa kuwasaidia zaidi ya waathirika 1000 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.

Hivi karibuni Risasi Jumamosi lilifika kituoni hapo na kujionea mazingira ya kituo hicho pamoja na kuzungumza na uongozi ambapo lilizungumza na mkurugenzi wa kituo hicho, Luis Botia ambaye ni raia wa Spain aliyekuja nchini tangu mwaka 2007.

Botia alifika nchini kwa mualiko binafsi lakini akajikuta ameingia kwenye kazi ya kuwasaidia waathirika wa madawa ya kulevya kazi aliyokuwa akiifanya nchini mwao. Botia anasema baada ya kufika nchini Tanzania, alishangazwa na wingi wa vijana waliojiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya hivyo Mungu aliwaingia mioyoni mwao na kuamua kuanzisha kituo hicho.

Amesema tangu kianzishwe mwaka 2007 mpaka sasa, kimeshawasaidia zaidi ya watu 1000; wavulana na wasichana kutoka katika mikoa mbalimbali nchini ambapo wengi walifanikiwa kuacha kabisa na wengine wanafika kituoni hapo kushukuru na wengine wanapiga simu.

KUJIUNGA NI BURE!

kituo hicho ambacho ni cha kipekee kutokana na huduma zake kuwa tofauti ukilinganisha na huduma za vituo vingine vya sober, Botia alieleza kuwa kwanza huduma zinazotolewa kituoni hapo ni bure.

“Hakuna malipo ambayo mteja inabidi alipie, akifika kituoni hapa atalala, kula na mambo mengine yote ikiwa pamoja na matibabu vyote ni bure. Mteja hatalipia hata senti moja kwa muda wote atakaokaa kituoni hapa,” anasema.

TARATIBU ZA KUJIUNGA

Botia alisema taratibu za kujiunga ni kwamba mteja anatakiwa afike kituoni au apige simu namba 0783413138 kwa wanaume na kwa wanawake 0712568773 au email info@ changamoto.org, lakini mteja anapaswa kuwa na picha ndogo mbili pamoja na namba ya simu ya ndugu au mtu anayemfahamu.

“Mteja akishajiunga kituoni hapa kitu cha kwanza itabidi kumpima afya yake kuangalia ameathirika kiasi gani au kama ana magonjwa ya kuambukiza inabidi aanzishiwe tiba mara moja ili asije kuleta madhara kwa wengine,” anasema Botia.

HUDUMA ZINAZOTOLEWA

Mbali na kutibu madhara ya madawa kwa kufanya mazoezi na mambo mengine, kituo hicho kimejikita kuwapa waathirika mafunzo ya kiufundi katika fani mbalimbali wawapo kituoni hapo ili kuwasaidia hata wanapotoka na kurudi katika familia zao waweze kujiajiri.

Botia alieleza kuwa nia ya kituo hicho ni kumfanya mteja kuachana kabisa na madawa ya kulevya na tabia chafu kutoka moyoni mwake. “Mteja afikapo kituoni hapa inapaswa aanze maisha mapya, abadilike kuanzia tabia n.k,” anasema Botia.

Anaongeza kuwa, wao hufundisha mtu abadilike kutoka ndani ya moyo na siyo nje ndiyo maana hawatoi dawa kwa ajili ya kupunguza matumizi isipokuwa wanamwachisha. Hairuhusiwi kutumia  sigara, pombe, bangi, madawa n.k kwa muda wote ambao mteja atakuwepo kituoni hapo.

MUDA WA KUKAA KITUONI

Botia alizidi kueleza kuwa muda wa kukaa kituoni hapo ni kuanzia miezi sita mpaka nane na kuendelea kutokana na hali ya mteja hata kama atataka kukaa zaidi, wanachozingatia ni kuona mtu amebadilika tabia kutoka moyoni mwake na kuhakikisha akitoka hapo anakwenda mtaani akiwa tofauti na alivyokuwa mwanzo.

HATUA ANAZOPITIA MTEJA

Botia anasema kuna hatua tatu anazopitia mteja akiwa kituoni hapo; hatua ya kwanza ni kumpokea mteja aliyeathirika na madawa ya kulevya.

“Hatua hii ni ngumu kidogo na inahitaji uangalizi wa hali ya juu kwa mteja kwani ni tofauti na vituo vingine ambavyo hawatoi dawa yoyote inayofanana kwa mteja bali ni kumwachisha moja kwa moja hivyo mteja anaweza kuwa katika hali ngumu ya arosto.

dawa

“Kuna kazi ya ziada ya kumpa moyo na kuwa naye karibu kwa muda wote hivyo mteja atakuwa anafanya kazi ndogondogo na mazoezi ya hapa na pale,” anasema. Kuhusu hatua ya pili, Botia alisema ni kuanza kumfundisha mafunzo ya ufundi wa fani mbalimbali zilizopo katika karakana zao, kwa mfano ufundi seremala, kuchomelea, kupaka rangi, kutengeneza milango, madirisha ya alumminiam, ujenzi n.k.

“Hiyo tunampa ili kumfanya asifikiri sana ili nao waweze kupata kazi ya kufanya na baadaye kupata ujuzi mpaka pale watakapo kuwa sawa,” anasema. Botia alizidi kueleza kuwa, awamu ya tatu ni kurudi mtaani.

“Awamu hii pia ni ngumu kidogo kwani baadhi ya wateja wanaenda kukutana na maisha waliyoyaacha mitaani, watakutana na vishawishi na marafiki ambao bado wanaendelea na tabia chafu pamoja na matumizi ya madawa hivyo mteja asipokuwa makini anaweza kurudia matumizi ya madawa hivyo kuna namna ambayo tunafanya kuwasaidia,” anasema.

*Risasi Jumamosi lilijionea mazingira ya kituo hicho yakiwa safi na viwanja vya michezo kuanzia mpira wa miguu, mpira wa wavu na mpira wa mezani. Pia kuna bustani na mifugo kama vile kuku, bata nk, inayohudumiwa na waathirika wenyewe. “Tunafundishwa kupendana, kushirikiana, kusaidia wengine, kusali ikiwa ni pamoja na kumjua na kumtumikia Mungu.

Tumetambua makosa yetu, tumetubu dhambi na sasa tumekuwa wapya, tumebadilika kuanzia mioyoni mwetu, matendo mpaka tabia,” alisema mmoja wa waathirika hao aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Meckion Mathew/GPL