×

Bossou Agoma Kucheza Yanga

Said Ally |CHAMPIONI| Dar es Salaam

IMEBAINIKA kwamba beki mgumu wa Yanga, Mtogo, Vincent Bossou alikuwa nyumbani kwake akishuhudia wenzake wakifungwa mbele ya Simba kwenye pambano la ligi kutokana na kugomea kuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo akishinikiza kulipwa stahiki zake.

Bossou anayejulikana kwa kucheza kwa nguvu na upambanaji, hakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichopoteza pambano lake dhidi ya Simba kwa mabao 2-1, mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar, juzi. Bossou aliyecheza michuano ya Afrika (Afcon) mwaka huu akiwa na timu ya Togo, ameliambia Championi Jumatatu kuwa aliangalia mechi hiyo kwa kutumia runinga akiwa kwake ambapo wenzake walipoteza kwa kipigo hicho.

“Mimi siumwi wala sina tatizo lolote lile ila sikucheza mechi hiyo na Simba kwa sababu kuna stahiki zangu ambazo sijalipwa bado na viongozi wamekuwa wakipiga chenga juu ya kulipwa kwangu kabla ya kwenda Afcon, ambapo malipo hayo ni ya miezi minne iliyopita.

“Niliamua kususia kucheza mechi hiyo na nyingine zinazokuja mpaka wanilipe stahiki zangu ambazo nazidai kwani inavyoonyesha kwamba fedha zilitolewa kwa sababu wengine wamelipwa vizuri lakini kwangu ndiyo kumekuwa na mambo hayo yanayojitokeza ya udanganyifu,” alisema Bossou.