
Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya ya Mkuranga.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema kuwa maendeleo ya wananchi wa Mkuranga yataletwa na wao wenyewe kwa kufanya kazi na kujituma.

Waziri Nape ameyasema hayo wakati wa Fainali ya Ulega Cup iliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule Msingi Mkuranga. Nape alisema licha ya michezo kuhamasisha umoja, mshikamano na furaha kwa jamii pia ametaka ihamasishe na shughuli zingine za maendeleo.

Amesema katika jitihada za Mkuranga kuwa na uwanja wa mpira atawaunga mkono baada ya kupata mchoro wa ramani ili wilaya hiyo iwe na uwanja utakaotumika kuchezea mechi mbalimbali hata za Ligi Kuu.

Nape akiwa katika picha ya pamoja na timu ya Tengera mkoani Pwani.
Katika fainali hiyo Waziri Nape amechangia shilingi laki tatu kwa timu tatu zitakazogawana laki moja kila timu kwa mshindi wa kwanza wa pili na watatu.

Nape Nnauye akiwa katika picha ya pamoja na timu ya Kisiju mkoani Pwani.
Hata hivyo, fainali hiyo imechezwa kati ya timu ya Kisiju na Tengerea ambazo zilitoka sare ya bila kufungana hadi zilikwenda katika hatua ya matuta na kuibuka kwa timu ya Tengera kwa mabao matatu dhidi ya timu ya kisiju iliopata magori mawili.

Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega akizungumza jambo.
Waziri Nape amesema mashindano yajayo atamuunga mkono mbunge kupata wadhamini wa mashindano ili kuendesha mashindano hayo Kwa ufanisi zaidi.

Nae Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega alisema vijana wameonyesha vipaji ambayo vinatakiwa kuendelezwa na kuweza vijana hao kufika kuchezea timu kubwa za ligi kuu.

PICHA NA MPIGA PICHA WETU | MKURANGA