
Na MWANDISHI| GAZAETI LA AMANI| KIJIWE CHA MC PILIPILI
NI Alhamisi nzuri tu leo, Mungu bwana bado anatupenda sana maana leo na mimi pia kama wewe, ameniamsha salama. Namshukuru sana. Unajua ukiamka salama lazima useme asante Mungu.
Nasema hivi kwa sababu, wewe umeamka mzima, kuna walioamka na kipindupindu! Oke…oke! Leo nataka kuzungumzia zaidi hizi simu za kisasa, wenyewe mnaita sijui smart phone. Smartphone bwana mimi naziona kama zimetengenezwa kwa ajili ya kuja kuvunja ndoa za watu hapa duniani au Ulaya au Afrika au Afrika Mashariki lakini zaidi sana Tanzania lakini zaidi sanasana, Dar es Salaam.

Juzi, jirani yangu mmoja alizozana na mkewe kisa chakula hakijaiva sasawasawa, sasa mimi nikawa nasikiliza huku najiuliza mama nanihii kweli kwa uzoefu wake wa ndoa kwa miaka kumi na mingapi sijui kweli anaweza kupika chakula hakijaiva?
Niliposikiliza kwa umakini nikagundua kumbe chakula chenyewe alikipika mdada wa kazi. Kwa wasiowajua wadada wa kazi ni wale wasichana wanaosaidia kazi za ndani.
“Sasa wewe mke wangu, dada wa kazi kaja juzi toka kijijini, unamwachia apike biliani ataliweza kweli?” baba mwenye nyumba alifoka. Akazidi kufoka bwana: “Kwanza kwa nini wewe mchana kutwa upo na simu tu, unachati na mwanaume gani?”
Hapo nikatega sikio ili nisikie vizuri majibu ya mama nanihii.
“Mume wangu sichati na mwanaume, naweka picha Instagram na Facebook. Kuna picha nilipiga jana nilipotoka saluni ndiyo naziposti.”
Mimi kusikia hivyo nikafurahi sana maana na mimi tatizo kubwa nyumbani kwangu ni hilo, sasa nilidhani nipo peke yangu tu kumbe tupo kibao.

Mimi tangu nimeoa ni mwaka wa saba sasa, mke wangu alishasema hataki kusikia habari za msichana wa kazi, nikasema huyu sasa ndiyo mke. Mh! Mwaka jana nilipomnunulia smartphone halafu akina mama nanihii wakamfundisha kuanzisha Instagram, Facebook,
wee! Wiki tu akaanza…
“Oooh! Kazi nyumbani ni nyingi sana, nataka msichana wa kusaidia kazi za ndani.”
Nikamletea! Anaitwa Tabu! Nilimtoa Iringa! Bwana…bwana! Badala ya dada kuwa msaidizi wa kazi za ndani, amekuwa ndiye mwenye kazi mwenyewe na mke wangu ndiye msaidizi sasa! Mke wangu kukicha tu, Facebook, Instagram, WhatsApp! Kwanza eti ananifundisha na mimi kuingia kwa sababu kuna umbeya mwingi.
Inafika wakati naamini kabisa kwamba, akiwa amelala hapati usingizi kuche ili aingie mitandaoni. Akipikiwa pilau na Tabu tu yeye katupia mtandaoni na maandishi juu; ‘mchana wangu wa leo uko hivi’.
Jumapili tukitoka kanisani tu, nje ya kanisa anamwomba kila mtu anampa simu yake ampige picha, anatupia, anasema; ‘Mkumbuke Mungu wako kama mimi.’ Yaani ni balaa na kero. Jamani wanawake punguzeni, mnaposema mnataka 50 kwa 50 iwe hivyo, mbona mnaonekana kama mnataka 95 kwa 5?
Na Mc Pilipili +255 715 415 542