
DAR ES SALAAM: Usafiri kafiri! Hali ya usafiri katika baadhi ya maeneo ya pembezoni mkoani Dar es Salaam ni mbaya, kiasi kwamba katika eneo la Kimara Mwisho, njia iendayo King’ong’o na Matosa, usafiri pekee wa Noah unawalazimisha wanafunzi kushindiliwa kwenye buti kama mizigo.

Katika nusanusa ya makamanda wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) mwishoni mwa wiki, katika eneo hilo la Kimara, walishangazwa baada ya kuona wanafunzi watano ‘wakishindiliwa’ katika buti la Noah hilo, ambalo katika siti zake za kawaida, abiria walikuwa wamejaa. Katika oparesheni hiyo, OFM walishuhudia kwa macho mchana kweupe wanafunzi wakishindiliwa kwenye buti kama mizigo huku wakitakiwa kutoa nauli kwanza kabla hawajapanda.

Kwa namna walivyokuwa wamejazana ni hatari kwa wanafunzi hao kama kupeana magonjwa ya kuambukiza na kukosa hewa ya kutosha. Wakizungumza na makamanda wetu, baadhi ya wanafunzi walisema kuwa wanakiona cha mtemakuni, kwani kila siku wanasafiri kwa kupakiwa kwenye buti, kwani madereva ambao pia ndiyo makondakta, wanakataa wasikae kwenye siti kama hawana nauli kamili ambayo ni shilingi mia tano.

“Kwa kweli tunapata mateso makubwa maana huku kwenye buti tunaminyana sana, tunapakizwa kama mizigo na kabla
ya kupanda lazima tutoe nauli kabisa, mateso yote haya ni kwa vile hatuna uwezo wa kulipa nauli kamili na hawa wenye magari ya Noah wanaona tukikaa kwenye siti wanapata hela ndogo maana siti zipo chache, tunamuomba Rais Dk. John Magufuli atusaidie,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.
Kwa upande wa baadhi ya wakazi na wasafiri wa maeneo hayo walieleza kuwa hali hiyo ya wanafunzi kushindiliwa kwenye buti imeshakuwa ni jambo la kawaida kutokana na tatizo la usafiri lililopo maeneo hayo huku wakilalamikia suala la kutokuwepo askari wa barabarani ‘trafiki’ kwenye njia hiyo.
“Tatizo kwenye hii barabara ya kuelekea King’ongo na Matosa hakuna askari jambo ambalo madereva wanalichukulia kama faida kwao kwa kuwapakiza wanafunzi kama mizigo, ukweli wanafunzi wanateseka kwani kama hawana shilingi 500 ya nauli hawawezi kukaa kwenye siti za kawaida ndiyo hivyo wanawekwa kwenye buti, tunaomba serikali iliangalie hili,” alisema abiria mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Musa.
Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Meya wa Ubungo, Boniphace Jacob ili kujua kama anajua adha wanazozipata wanafunzi hao, lakini simu yake ya mkononi iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu.