×

R.O.M.A Sasa Kama Nas



Makala: Boniphace Ngumije | RISASI JUMATANO| RISASI VIVES

MAPEMA mwanzoni mwa miaka ya 2000 baada ya dunia kushuhudia ‘battle’ ya wakali wa Hip Hop Marekani, Nasir Jones ‘Nas’ na Shawn Carter ‘Jay Z’ kila mmoja akidai ni mfalme wa aina hiyo ya muziki duniani, Steve Stoute, aliyekuwa bosi ndani ya Kampuni ya Sony, alimvuta Nas pembeni na kumpa mchongo wa pesa!

Akiamini kuwa Nas ni mkali zaidi ya Jigga, Stoute ambaye amewahi kuzungumza wazi kwenye kipindi cha redio maarufu Marekani cha Sway In The Morning juu ya hisia zake hizo, aliamini tuzo ya ufalme wa uandishi bora wa mashairi aliyokuwa ametunukiwa Nas, ilikuwa ni sahihi kabisa.

Nasir Jones ‘Nas’

Stoute hakutaka Nas awe na heshima pekee kama mkali wa mashairi, bali alitaka abadili maisha yake na kuwa tajiri kutokana na kipaji chake.

Baada ya kukaa chini na kufanya mazungumzo ya kina, Nas akakubaliana na Stoute, akaachana na nyimbo za Hip Hop, akaanza kuimba, kitu kilicho-mpatia umaarufu dunia nzima pamoja na pesa za kutosha, licha ya ukweli kwamba Jay Z yupo juu zaidi yake kibiashara.

Kama ilivyokuwa kwa Nas ndivyo, ilivyo kwa mwanamuziki mwenye ‘utitiri’ wa mashabiki Bongo, Ibrahimu Mussa ‘R.O.M.A Mkatoliki’.

Tofauti yao ni kwamba, Roma, aliyejijengea heshima kubwa Bongo kwa kuimba nyimbo zenye ujumbe mzito, akiikosoa serikali, wadau wa muziki, taasisi binafsi, watu na mambo mengine mengi, kwa hiyari yake mwenyewe, ameamua kupiga chini aina ya utungaji na uundaji wa muziki, hivyo kuanza kuimba nyimbo zinazoweza kumpa mafanikio makubwa kifedha kuliko ilivyo hivi sasa.

Roma kwa kauli yake mwenyewe akizungumza na Risasi Vibes, amesema muziki aliokuwa akiufanya nyuma, licha ya kumpa mafanikio makubwa, unamzuia kukua na kupaa mbali kiasi cha kufikia levo za kimataifa.

Roma ameamua kubadilika kama Nas ili apige mkwanja na kufikia malengo yake ya kimuziki. Kwa hiyo mrengo wa mashairi kama aliyoimba kwenye ngoma za Mr. President, Karibu Kwenye Kalamu, Viva Roma, Mathematics, Mwanakondoo na 2030 ndiyo basi tena!

Yaani mashabiki wake watapata ladha hizo kwa nadra au wanaweza wasipate kabisa na wakaishia kusikiliza aina ya uandishi wake mpya wa mashairi kama aliyofanya kwenye nyimbo kama K aliomshirikisha Baghdad na Snura pamoja na Msimsahau Mchizi aliofanya na Moni wa Kundi la Centro Zone la Dodoma.