Na Mwandishi wetu/CHAMPIONI/GPL
NIANZE makala yangu ya leo kwa kumpa pongezi mbunge Nape Nnauye ambaye alikuwa waziri kabla ya uteuzi wake kutenguliwa wiki jana.
Akiwa waziri mwenye mamlaka katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape ameondoka lakini nyuma ameacha sifa nyingi kubwa na ndiyo maana hata utenguzi wake ulionekana kuwagusa wadau wengi.
Sina maana napinga maamuzi ya mamlaka iliyotengua uamuzi wake lakini kwenye ukweli lazima tuseme, hivyo nampa pongezi Nape kwa kazi nzuri aliyoifanya, pia nimkaribishe kaka yangu na mzee wangu Harrison Mwakyembe katika wizara hiyo.
Naamini kwa uzoefu alionao kwa mamlaka aliyonayo Mwakyembe ataanzia pale ambapo Nape aliishia kisha ataendeleza kasi ileile na ikiwezekana kwa nguvu kubwa, binafsi najua wadau wengi wapo tayari kumpa ushirikiano kama walivyompa Nape, japokuwa hilo litategemea na yeye mwenyewe katika utendaji wake.
Baada ya hapo niipongeze timu ya taifa Taifa Stars kutokana na kuwa na mwendo mzuri baada ya kukabidhiwa kwa kocha mzawa, Salum Mayanga. Nimeandika makala haya kabla ya mchezo wa jana wa Stars dhidi ya Burundi lakini kwa kile ambacho kilifanywa na Stars kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Botswana bila shaka kilikuwa kizuri.
Wapo walioanza kutoa maneno kuwa Botswana siyo kipimo kizuri kwa Stars, lakini niwakumbushe tu kuwa katika dunia ya sasa ambayo vitu vingi vinakuwa wazi kirahisi, timu nyingi zinaboreka na hata wapinzani wetu hao wapo vizuri zaidi yetu katika viwango vya ubora.
Tanzania tumekuwa katika mtikisiko kwa muda mrefu, timu yetu ya taifa imeonekana kukosa mwelekeo, sasa kunapojitokeza utulivu kama huo ni vema tukautumia vizuri kwa lengo la kukuza soka letu na kuonyesha njia sahihi kwa wachezaji wetu.
Nikiyaweka hayo kando, mada yangu kubwa ya leo ni kuhusu wachezaji wa kimataifa katika ngazi ya klabu zetu ambapo kama tunavyofahamu kuwa kanuni zinaruhusu wachezaji saba, lakini tunatakiwa kujiuliza kanuni hiyo inatusaidia au inatupoteza zaidi?
Awali walikuwa wachezaji watano baadaye ikaamriwa iwe saba, hapo kati kuliwahi kuwa na mjadala wa kupunguza na wengine walitaka kanuni iruhusu waongezwe, nikajiuliza kabla ya kufanya maamuzi hayo tunajua tunachokifanya?
Jibu ni kuwa dunia ya sasa kweli huwezi kuishi peke yako kama kisiwa, lazima ujichanganye na wachezaji wa mataifa mengine ili upate changamoto, lakini pamoja na hivyo tunatakiwa kujiuliza majaaliwa ya wachezaji wetu na mwelekeo wa taifa kwa jumla.
Nitoe mfano hai, ukitazama kikosi cha Yanga katika miaka ya hivi karibuni kimekuwa kikifanya vizuri ndani ya Tanzania lakini kwa asilimia kubwa wachezaji ambao wamekuwa wakitamba ni wale wa kimataifa.
Wazawa wamekuwa wanapata nafasi lakini wanaonekana kumezwa na wageni, mfano sasa hivi Simon Msuva ndiye mchezaji mzawa ambaye anaonekana kung’ara kikosini hapo kuliko wazawa wengine.
Ukitazama klabu kubwa za Tanzania, nikianza na hiyo Yanga, Simba na Azam FC zote zimekuwa zikitumia nguvu kubwa kusajili wachezaji wa kigeni, hao ndiyo ambao wanakuwa wanatamba huku wazawa wakionekana kukosa nguvu ya kushindana nayo.
Sikatai wageni lakini nahisi kuna kitu au mipango inatakiwa kufanyika ili kuwafanya wachezaji wazawa nao wakawa na nafasi ya kupambana nao, ama kwa kupewa kipaumbele au kuelezwa nini ambacho kinatakiwa kufanyika na isionekane wageni ndiyo wanaotakiwa kutawala soka.
Nasema hivyo kwa kuwa najua anguko la wachezaji wazawa ndilo anguko la timu ya taifa, tukiruhusu wageni watutawale kwenye ngazi ya klabu, wakafanya kazi nzuri huku wazawa wakiwa wasindikizaji matokeo yake ni kuwa na timu ya taifa nyepesi.
Tanzania tuna vipaji vingi tu ambavyo kama hakutakuwa na njia ya kuvikuza tukisubiri vijikuze vyenyewe tutaendelea kufeli, lakini kukiwa na mpango sahihi ya kuviboresha, katika wachezaji 10 lazima tutapata watano au sita na watakuwa faida kwa taifa.