
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, leo amezindua ujenzi wa barabara ya kutoka Pugu mpaka Majohe kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita saba.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Mjema ameeleza kuwa serikali imeamua kuzindua ujenzi huo baada ya kupata malalamiko kuwa wananchi wamekuwa wakipata adha kubwa ya usafiri kwani barabara hiyo imekuwa haipitiki kipindi cha mvua na kusababisha kujaa maji ambapo ujenzi huo unatarajiwa kuchukua muda wa miezi mitatu mpaka kukamilika kwake.

Pia ametoa tahadhari kwa wanaoishi kwenye hifadhi ya barabara kubomoa nyumba zao mara moja kabla serikali haijachukua hatua, huku akisisitiza kuwa hakutakuwa na fidia yoyote kwa watakaobomolewa.

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo ametembelea dampo la Pugu-Kinyamwezi na kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wakazi waishio eneo hilo kuhusu miundombinu mibovu ya dampo hilo ambalo limekuwa likitiririsha maji machafu kuelekea kwenye makazi yao.
Akijibu kero hiyo, Mjema amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuziba matundu yote yanayotiririsha maji machafu kwenye makazi ya wananchi hao, huku wakisubiri utaratibu kutoka Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) na kuwataka wawe na subira ana akatoa wito kwa wanaoishi mabondeni kuhama mara moja na kwamba serikali itawapatia maeneo mengine ya kuishi.