×

Caf Washikilia Mkataba wa Mkude

Na Khadija Mngwai | CHAMPIONI|GPL
MICHUANO ya kimataifa inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) imemzuia kiungo wa Simba, Jonas Mkude kusaini mkataba na klabu hiyo mpaka pale atakapohakikisha anaifanikisha timu yake kupata tiketi ya kushiriki michuano hiyo.
Mkude ni miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao wanatarajia kumaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu mara baada ya ligi kumalizika ambapo hadi sasa hajafanya mazungumzo yoyote.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkude amesema mtazamo wake wote kwa sasa ni kuona timu yake inafanikiwa kushiriki michuano ya kimataifa mwakani kwa kupata nafasi ya uwakilishi kupitia ligi kuu au Kombe la Shirikisho (FA), kisha ndiyo aanze mchakato wa kukutana na mabosi wa Simba.
“Simba haijashiriki michuano ya kimataifa kwa muda, hivyo siyo kitu kizuri na tunachokiangalia hivi sasa ni kuona ni jinsi gani tunaweza kufanikiwa kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
“Kuhusu kulegeza kamba katika matakwa ya mkataba wangu jambo hilo halipo, ila kilichopo hivi sasa ni kuona ni jinsi gani timu itapata nafasi hiyo ya uwakilishi kimataifa na baada ya hapo ndio nitapata nafasi ya kukutana na viongozi kwa ajili ya kujadili mkataba wangu mpya wa msimu ujao, kwa sasa kila mmoja yupo bize kuhakikisha timu inafanya vyema,” alisema.

Leave a Comment