
KIKOSI cha timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys, kipo nchini Cameroon kwa ajili ya kambi ya mwisho kabla ya kwenda Gabon kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17.
Serengeti Boys kabla ya kufika Cameroon, ilikuwa Morocco ambapo pia iliweka kambi, ambapo ikiwa huko ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Gabon na yote kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Jana Jumapili ilitarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya vijana wenzao wa Cameroon. Serengeti Boys inajaribu kucheza na timu hizo ili kujiweka fiti kabla ya kuanza kwa michuano hiyo inayotarajiwa kuanza kuunguruma Mei 14, mwaka huu huko Gabon.
Kucheza na Ghana, Gabon na Cameroon ambazo zote zitashiriki michuano hiyo zikiwa Kundi A, ni jambo zuri kwa vijana wetu kwani watakuwa tayari washajua kwa kiasi fulani wanakwenda kukutana na timu za aina gani.
Ikumbukwe kuwa Serengeti Boys wao wamepangwa Kundi B sambamba na timu za Niger, Ethiopia na Angola.
Matarajio ya Watanzania wengi ni kuona vijana wetu hao wakifanya vizuri kwenye michuano hiyo ikiwezekana kurudi na kombe hapa nyumbani baada ya kuwa na mwenendo mzuri kuanzia kwenye mechi zao za kirafiki mpaka zile za kufuzu michuano hiyo.
Lakini tunatakiwa kukumbuka kuwa katika michuano hiyo wanayokwenda kushiriki watakutana na timu za aina mbalimbali ambazo zingine zimetupita sana kisoka hasa soka la vijana. Miongoni mwa nchi hizo ni Ghana na Cameroon ambazo zote tumecheza nazo mechi za kirafiki.
Huku tukiwa na imani kubwa juu ya vijana wetu hao kufanya vizuri, itakapotokea wameshindwa kufanya kile tunachokitarajia, basi asitokee mtu au kikundi cha watu kuanza kuwalaumu.
Muda mwingine lawama zinatakiwa kwenda kwa wanaowasimamia, hapa namaanisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo ndilo lenye dhamana ya kuhakikisha soka letu linapiga hatua kwa njia sahihi.
Nchi kama ya Ghana au Cameroon, kwa muda mrefu zimejipanga kisoka tangu kuanzia ngazi ya chini, yaani soka la vijana kwa kuwaweka vijana wao katika akademi nyingi zilizopo nchini mwao.
Hapa kwetu utamaduni huo kwa muda mrefu haupo japo hivi karibuni kidogo ndiyo umeanza kwa kutengenezwa akademi ambazo zinalea vijana wetu.
Ukiangalia kikosi cha vijana cha Ghana chenye wachezaji 25 ambacho kimetangazwa kushiriki michuano ambayo Serengeti Boys nao wanaenda kushiriki, kuna wachezaji baadhi yao wanacheza timu za ligi kuu huko kwao na wengine wapo madaraja ya chini.
Ukiwaondoa hao, wapo wanaotokea kwenye akademi mbalimbali huko Ghana. Sasa hapo inakupa picha kwamba wenzetu wana kikosi cha aina gani.
Nilipongeze Benchi la Ufundi la Serengeti Boys chini ya Kocha Mkuu, Bakari Shime na mkurugenzi wa benchi hilo, Msweden, Kim Poulsen kwa kuwaweka pamoja vijana wetu kambini kwa muda mrefu hali ambayo inaweza kuwa faida kwao kwa kujiona kama vile wapo kwenye akademi.
Hivyo basi, kutokana na kutokuwa na misingi imara ya kisoka ndani ya nchi yetu, tusije kuwalaumu Serengeti Boys wakishindwa kutamba huko Gabon.