
Musa Mateja | CHAMPIONI | Dar es Salaam
KIUNGO mkabaji wa Azam FC, Himid Mao, juzi Jumatatu alikwea pipa na kutimkia zake Denmark kufanya majaribio na timu moja ya nchini humo ambayo inahitaji huduma yake.
Himid ambaye kwa muda mrefu alikuwa akitakiwa na timu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, amechagua kwenda Denmark kutokana na kuamini kwamba ndiyo sehemu sahihi kwake kutimiza ndoto zake.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema mbali na Himid kuna wachezaji wengine sita wanatakiwa kwenda nje ya nchi kufanya majaribio ambao wote wataondoka muda wowote kuanzia sasa.
“Himid ameenda Denmark kufanya majaribio ya siku kumi, lakini hiyo timu iliyomtaka ambayo kwa sasa inabaki kuwa siri yetu walitaka majaribio hayo yawe ya wiki mbili, tukaona si sahihi. Kuondoka kwake tayari tumeanza mchakato wa kutafuta mbadala wake kwani tunaamini hatutakuwa naye tena msimu ujao.
“Mbali na yeye, kuna wachezaji wengine kama sita hivi kutoka ndani ya kikosi chetu wanatakiwa kwenda nje ya nchi kufanya majaribio, muda ukifika tutawajuza ni kina nani na wanakwenda wapi,” alisema Kawemba.
Naye Himid alisema: “Watanzania waniombee niweze kufanikiwa katika majaribio yangu.”