SIMBA wana jeuri kubwa ya kwenda Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kwani imebainika kuwa kama wakienda kushtaki kwa shirikisho hilo, kanuni itawabeba na itakuwa ni uhakika kurejeshewa pointi tatu walizopokwa na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Simba, hivi karibuni ilipokwa pointi tatu na kamati hiyo, siku chache baada ya Kamati ya Saa 72 kuwapa pointi hizo kwa kubaini kuwa Kagera Sugar walimchezesha beki Mohammed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mchezo dhidi yao ambao walifungwa 2-1.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Champoini Ijumaa imezipata kutoka ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF, Simba itarejeshewa pointi hizo kama ikienda Fifa. Mtoa taarifa huyo alisema, kwa mujibu wa Kanuni za Fifa, ripoti inayotoa uamuzi wa matukio ya ndani ya uwanja ni ya mwamuzi wa kati anayepuliza filimbi.
Aliongeza kuwa, kamati hizo zote mbili zilizokaa katika vikao vyake, ripoti ya mwamuzi wa kati Jimmy Fanuel inasema alitoa kadi ya njano kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya African Lyon uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera, hivyo inamaamisha kuwa Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano ambapo nyingine alizipata katika mechi dhidi ya Mbeya City na Majimaji.
“Siku zote Fifa inatoa uamuzi wake wa ndani ya uwanja kwa kuifuata ripoti ya mwamuzi wa kati anayepuliza kipyenga na siyo mtu mwingine yeyote. “Kwa maana hiyo, upo uwezekano mkubwa wa Simba kurejeshewa pointi zake walizopokwa na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ya TFF ambazo awali walipewa na Kamati ya Saa 72 ya TFF.
“Ripoti iliyotolewa na mwamuzi wa kati, inasema kuwa, mechi na African Lyon alitoa kadi moja ya njano na kufikisha kadi ya tatu huku ripoti ya kamisaa na mshika kibendera mmoja zikionyesha Fakhi hakupewa kadi katika mchezo huo.
“Kwa maelezo hayo, moja kwa moja Simba watarejeshewa pointi hizo tatu walizochukuliwa kwa kupitia kanuni za Fifa ambazo humuamini mwamuzi wa kati pekee anayetoa kadi,” alisema mtoa taarifa huyo. Simba kwa kupitia rais wa klabu hiyo, Evans Aveva, juzi ilitangaza kwenda Fifa mara baada ya kukabidhiwa barua kutoka TFF ya kupokwa pointi hizo.
Hadi sasa zikiwa zinaelekea kukatika wiki mbili baada ya Simba kupokwa pointi, TFF haijaikabidhi Simba barua ya maamuzi hayo, huku ikielezwa kuwa shirikisho hilo linaogopa kufanya hivyo, kutokana na kupata vitisho kutoka kwa baadhi ya wajumbe wake wa kamati ya utendaji. Simba ikiwa imepokwa pointi, inaongoza ligi ikiwa na pointi 59 ikifuatiwa na Yanga yenye 56.