×

TGNP Yawapa 5 Wanafunzi wa Kike Elimu ya Juu

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Mtandao wa Wanawake Tanzania (TGNP)  umesema kuwa tatizo linalowakabili wasichana wengi hapa nchini ni changamoto ya masuala ya mapenzi wakiwa vyuoni ambapo husababisha kushindwa kumaliza masomo yao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, wakati wa hafla ya kuwapongeza wasichana 38 waliofanya vizuri katika elimu ya juu, alisema wanawake wengi wanashindwa kufikia malengo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kujiingiza katika masuala ya mapenzi wakiwa bado shuleni na kuwa na mtazamo wa kwamba wao ni wanyonge.

Baadhi ya wasichana wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini waliohudhuria hafla hiyo wakifuatilia kilichokuwa kikiendelea.

Amesema kuwa wanawake wanaonekana daraja la pili hali ambayo inafanya kuendelea kuweka mfumo dume wa maamuzi kufanywa na wanaume.

Liundi amefafanua kuwa wasichana ambao wamefanya vizuri  kwenye vyuo mbalimbali wanaonesha ukombozi wa wanawake katika kuleta maendeleo ya mwanamke mwezie.

Aidha aliongeza kuwa TGNP Mtandao imekuwa katika mstari wa mbele katika kuendesha harakati za kumkomboa mwanamke katika changamoto mbalimbali.

Hafla ya kuwapongeza ikiendelea.

Mmoja wa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji, Aisha Soudy  akizungumza katika hafla hiyo alisema wasichana wanazo changamoto nyingi ikiwemo mila na tamaduni ambazo humpendelea mtoto wa kiume huku mtoto wa kike akionekana asiyeweza kufanya kitu.

Naye mhitimu aliyefanya vizuri katika matokeo ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Sara Mgonela alieleza kwamba   msichana ana nafasi yake kama  akijitambua anachokifanya katika jamii yake.

Sara amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto kama mtoto wa kike lakini aliweza kufanya vizuri na kuwataka wasichana kujiamini kuwa wanaweza na kuwa na bidii.

Na Denis Mtima/GPL

Leave a Comment