
LICHA ya mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma kuonekana siyo lolote mbele ya mashabiki wa timu hiyo kutokana na kushindwa kuonyesha makeke yake, lakini mabao mawili aliyofunga mpaka sasa yanambeba.
Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Yanga msimu wa 2015/2016, akitokea FC Platnum ya nyumbani kwao, msimu wake huo wa kwanza alifanikiwa kufunga mabao matatu katika mechi nne za kwanza.
Ngoma alifunga mabao hayo katika mechi tatu za kwanza mfululizo dhidi ya Coastal Union, Tanzania Prisons na JKT Ruvu huku akishindwa kufunga bao katika mchezo wake wa nne dhidi ya Simba ambao Yanga walishinda kwa mabao 2-0.
Katika msimu uliopita, kwenye mechi nne za kwanza, Ngoma alifunga bao moja tu kwenye mechi dhidi ya Mwadui ikiwa ni tofauti na msimu huu ambapo ameweza kuvunja rekodi yake ya msimu uliopita kwa kufunga mabao mawili katika mechi nne za kwanza alizocheza mpaka sasa.
Mabao yake mawili ya msimu huu ameyafunga katika mchezo dhidi ya Lipuli mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 na dhidi ya Majimaji ambao ulimalizika kwa sare kama hiyo.
Hii inamaana kuwa Ngoma ameshawapa Yanga pointi mbili msimu huu hadi sasa, na ni picha kuwa michezo aliyofunga yote imemalizika kwa sare ya bao 1-1.
Ibrahim Mussa, Dar es Salaam