×

Mtoto wa Amina Chifupa: Nimebaki Peke Yangu

Stori: Boniphace Ngumije | IJUMAA WIKIENDA

DAR ES SALAAM: Inauma sana! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia kauli aliyoitoa mtoto Abdulrahman Mohamed Mpakanjia ambaye ni mtoto wa aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), marehemu Amina Chifupa, kuwa amebaki peke yake kufuatia kifo cha babu yake, Luteni Hamis Chifupa.

Abdulrahman Mpakanjia akishiriki mazishi ya babu yake.

Mzee Chifupa alifariki majira ya saa mbili za usiku wa Ijumaa iliyopita Upanga jijini Dar na kuibua simanzi nzito.

Abdulrahman akilia kwa huzuni kumpoteza babu yake.

Akizungumza kwa majonzi nyumbani kwa marehemu babu yake, Mikocheni B, Dar ambako ndiko msiba ulipowekwa, Abdulrahman alisema kuwa, tangu mama yeke afariki dunia mwaka 2006 na baba yake mzazi Mohamed Mpakanjia aliyekuwa mfanyabiashara maarufu kufuata mwaka 2009, amekuwa akiishi na kushirikiana katika mambo mengi na babu yake huyo, lakini jambo la kusikitisha zaidi na yeye amefariki dunia na kumuacha peke yake.

Luteni Hamis Chifupa enzi za uhai wake.

“Kiukweli ninaumia sana moyoni. Babu yangu ndiye alikuwa amebaki kuwa kila kitu kwangu. Ndiye alikuwa mama na baba kwangu, lakini sasa na yeye ameondoka na kuniacha peke yangu. Naye amewafuata wazazi wangu, kiukweli sijui tu maisha kwangu yataendelea vipi,” alisema kijana huyo huku akibubujikwa machozi na kuongeza:

 

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete akimpa pole Abdulrahman.

“Kama si kwa mapenzi ya Mungu, nisingehitaji kabisa babu aondoke maana ndiye alikuwa faraja yangu kubwa, sitasahau ukaribu wetu, utani na namna alivyokuwa ananisisitizia kusoma kwa bidii. Ukweli ni kwamba msiba huu unaniuma mno, lakini sina budi kuruhusu kila kitu kuendelea kama kilivyo.”

Amina Chifupa enzi za uhai wake.

Mbali na kifo hicho cha babu yake na wazazi wake, Abdulrahman amekwishawapoteza bibi yake ambaye ni mke wa Mzee Chifupa aliyefariki mwaka 2011, babu yake kwa upande wa baba na amembakiza bibi yake pekee ambaye ni mama wa baba yake.

Mohammed Mpakanjia enzi za uhai wake.

Naye Rashid Issa, mdogo wa marehemu Mzee Chifupa, akizungumzia tatizo hasa lililosababisha kifo cha mzee huyo alisema kuwa, Mzee Chifupa alianza kusumbuliwa na maradhi ya Kiharusi tangu Jumatano ya Mei 16, mwaka huu.

“Nikiwa Tabora nilipigiwa simu na mmoja wa wajukuu zangu kuwa kaka (Mzee Chifupa) alizidiwa na kudondoka kisha kupooza upande mmoja.

“Niliwataka wampeleke hospitalini na kweli walifanya hivyo siku iliyofuata ambapo walimpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikoanza matibabu na baada ya siku kadhaa alipopata nafuu, tulimtoa na kumpeleka Upanga, Dar kwa mwanaye wa kike,” alisema Issa.

Rashid Issa, mdogo wa marehemu Mzee Chifupa (katikati) akifafanua jambo msibani hapo.

Alifunguka kuwa, Mzee Chifupa aliendelea vizuri, lakini hali yake ilibadilika zaidi Ijumaa iliyopita ambapo alianza kulalamika kuwa hapumui vizuri na majira ya saa mbili za usiku alifariki dunia.

“Kwa familia nzima hili ni pigo kubwa. Lakini hatuna budi kukubaliana na ukweli, kuhusu taratibu za mazishi zitawekwa wazi baada ya baadhi ya watoto wake ambao wapo nje ya jiji hili (Dar) kufika msibani na kujadiliana,” alisema Issa.

Alimaliza kwa kusema kuwa Mzee Chifupa ameacha watoto zaidi ya thelathini na wajukuu wengi.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Amina!

ILIKUPITA HII? LIVE: Mazishi ya Baba wa Amina Chifupa Makaburini Kisutu, Dar

Leave a Comment